Wa FIFA; Wakala Alhaj Yussuf |
Na Mahmoud Zubeiry, IMEWEKWA MEI 19, 2013 SAA 6:20 MCHANA
WAKALA wa wachezaji anayetambuliwa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), Alhaj Yussuf Said Salim Awadh Bakhresa amesema kwamba alivutiwa mno na uchezaji wa viungo wa Yanga, Athumani Iddi ‘Chuji’ na Frank Domayo katika mchezo wao wa jana dhidi ya Simba SC.
Katika mchezo huo wa kufunga pazia la Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Yanga ilishinda mabao 2-0 yaliyofungwa na Didier Kavumbangu dakika ya tano na Hamisi Kiiza dakika ya 62.
Akizungumzia mchezo huo, Yussuf ambaye familia yake inaimiliki timu ya Azam FC, alisema kwamba pamoja na kuwa wachezaji wa timu zote walicheza vizuri, lakini yeye alivutiwa zaidi na Chuji na Domayo.
Yussuf, aliyewahi kumpeleka West Ham United Mrisho Ngassa akiwa Yanga kufanya majaribio, alisema kwa mchezo wa jana ulikuwa mzuri na dalili nzuri kwa soka ya Tanzania kwa ujumla.
“Mechi za ushindani kama hizi ndizo zinakuza viwango vya wachezaji na timu. Na hii ni faida kwa soka ya Tanzania. Ndiyo maana kila siku tunapigania ushindani zaidi katika Ligi Kuu ya nchi hii,”.
“Ligi ikiwa ya ushindani, wachezaji watakuwa bora hata sisi mawakala itakuwa kazi rahisi kwetu kuwanadi wachezaji wetu. Kwa kweli napongeza sana timu zote, hasa washindi Yanga,”alisema Yussuf.
Yussuf alisema Yanga walistahili kushinda kwa sababu walicheza vizuri kuliko wapinzani wao na akampongeza pia refa Martin Saanya kwa kuumudu mchezo huo.