Pichani ni Ben Mwaipaja, Mwenyekiti wa Manyara Press Club, ambao wamewatimua wanachama wao akiwemo mwakilishi wa ITV na Radio One mkoani Manyara
Na. Mwandishi wetu
Babati
Waandishi watatu wa Klabu ya waandishi wa habari wa Mkoa wa
Manyara, Mamec, wamevuliwa uanachama wao kutokana na kukosa maadili baada ya
kufunga kwa kufuli ofisi ya klabu hiyo.
Uamuzi huo mgumu ulichukuliwa
juzi mjini Babati na wanachama wa Mamec baada ya kusomewa na Mwenyekiti wao
Benny Mwaipaja uamuzi wa kamati ya maadili iliyopendekeza wachukuliwa hatua
baada ya wao kugoma kufika.
Wanachama hao waliwafutia uanachama ni Charles Masayanyika wa
kituo cha ITV na Radio One, Hamida Khalid wa gazeti la Tanzania Daima na na
Tabia Daffo wa Radio Uhuru.
Ilidaiwa kuwa, wanachama hao watatu walifunga ofisi ya Mamec,
Novemba mosi mwaka huu wakidai kuwa hawautambui uongozi uliopo hivyo uamuzi
uliotolewa ni kuwafutia uanachama kutokana na kukosa maadili
“Waandishi hawa waliitwa kwenye kamati ya Maadili, Usuluhishi na
Nidhamu lakini wakagoma kufika hivyo kamati hiyo ikapendekeza wapewe onyo au
adhabu ambayo wanachama wanaona inafaa,” alisema Bw Mwaipaja.
Pia, wanachama hao walikubali kwa
ridhaa yao kujiuzulu kwa Katibu Mtendaji wa Mamec, Zacharia Mtigandi wa Star
TV, aliyeandika barua ya kujiuzulu ambapo nafasi yake itashikiliwa na Abraham
Mlundi wa gazeti la Mwanajamii.
Pamoja na hilo wanachama hao waliridhia kujiuzulu kwa mjumbe wa
kamati tendaji, Hamida Khalidi ambapo nafasi yake ilijazwa na Joseph Simba wa
gazeti la Mwanajamii.
Makamu Mwenyekiti wa Mamec, Mary
Margwe alisema hatua hiyo ya kuwafukuza uanachama waandishi hao imechukuliwa
ili kuleta nidhamu kwenye chama na watachukua hatua kali endapo hali hiyo
itajitokeza tena.
“Bora tubaki wanachama wawili wenye malengo ya kutumikia jamii
kwa ufasaha kuliko kuwa na kundi kubwa la wanachama, sisi tupo 17 tu lakini
tunaanza kufunga ofisi badala ya kuleta hoja mezani,” alisema Margwe.
Hata hivyo, wanachama wa Mamec,
wamepongeza hatua hiyo ya kufukuzwa uanachama waandishi hao watatu kwani ni
muda mrefu walikuwa wanasababisha fujo zenye lengo la kuanzisha migogoro.
MWISHO.