Barabara mpya ya Lami inayounganisha Tanzania na nchi ya Burundi kutokea mjii Kigoma |
Mkoa wa Kigoma umeazimia kumwandikia Barua ya pongezi na
shukurani Rais Jakaya Kikwete kwa kuwezesha mkoa huo kupata barabara za lami
zinazotarajiwa kuunganisha mkoa huo na mikoa mingine ya Tanzania pamoja na nchi
za jirani
Azimio hilo limefikiwa wiki hii mjini Kigoma wakati wa kikao
cha Bodi ya Barabara baada ya wajumbe wa Bodi hiyo kubaini kuwa serikali ya
awamu ya nne imedhamiria kuufingua mkoa huo kwa njia ya kujenga na kuimarisha
miundombinu hususani barabara
Akitoa tamko hilo la dhamira ya kumshukuru Rais Mkuu wa mkoa
wa Kigoma ambaye pia ni mwenyekiti wa Bodi ya barabara mkoani humo kanali
Mstaafu Issa Machibya amebainisha kuwa serikali imeonesha dhamira ya kuimarisha
miundombinu ili kupanua uchumi wa mkoa na taifa
Kwa upande wake meneja wa Tanroads mkoa wa Kigoma mhandisi
Narcis Choma amebainisha kuwa kwa sasa mkoa wa Kigoma una kiasi cha kilomita 1,205.38
za barabara zote katika mkoa mzima
Mhandisi Choma amefafanua kuwa katika urefu wa barabara hizo
ni kilomita 182.54 pekee ndizo zimejengwa kwa kiwango cha lami wakati kilimita
1,040.44 ni za changarawe na udongo.
Aidha katika kikao hicho, wenyeviti wa halmashauri za wilaya
za Kakonko na Kasulu Bw. Juma Maganga na William Luturi wamempongeza meneja wa
TANROADS Kigoma kwa utendaji mzuri wa kazi za ufuatiliaji na usimamizi wa
ujenzi wa Barabara
Hata hivyo wenyeviti hao wameiomba serikali kuwekeza katika
ujenzi wa barabara kuu ya kutoka Kidahwe hadi Nyakanazi na kusisitiza kuwa
pamoja na kurahisisha mawasiliano, barabara hiyo ndiyo inayohusika na uchumi wa
wanakigoma tofauti na ile inayojengwa kutoka Kigoma kwenda Tabora ambako sehemu
kubwa ya eneo hilo ni msiti wa hifadhi
Wamesisitiza kuwa barabara ya Kigoma, Kasulu, Kibondo,
Kakonko hadi Nyakanazi ndiyo barabara muhimu kwa uchumi wa mkoa wa Kigoma
kutoka na kile kinachotajwa kuwa inapita katika makazi ya watu na eneo la soko
la mazao ya mashambani.