Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya
Mbozi, Dk Charles Mkambachepa juzi alionja joto la jiwe baada ya Katibu Mkuu wa
CCM, Abdulrahaman Kinana kumtaka arudishe haraka Sh209 milioni za Saccos
ya Chama cha Walimu zilizochukuliwa na halmashauri hiyo katika mazingira ya
kutatanisha kuanzia Mei mwaka huu.
Hali hiyo ilijitokeza juzi jioni wakati Kinana
alipozungumza na baadhi ya watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi hususan
walimu.
Dk Mkambachepa alilazimika kutamka wazi kwamba
atahakikisha anawalipa fedha zote ifikapo mwishoni mwa Januari mwaka ujao na
kwamba juzi hiyo aliwalipa zaidi ya Sh32 milioni kupunguza deni hilo.
Awali Kinana alipokea taarifa ya malalamiko
lukuki ya walimu yakiwamo ya madai ya zaidi ya Sh1 bilioni na pia halmashauri
kuchukua Sh209 milioni za makato ya walimu kwa ajili ya kurudisha mikopo ya
Saccos.
Walimu walidai halmashauri hiyo chini ya
Mkurugenzi mstaafu Edson Chelewa ilichukua fedha hizo ikidai zinatumika katika
masuala ya kumpokea Rais Jakaya Kikwete kwenye sherehe za Mei Mosi
zilizofanyika kitaifa mkoani Mbeya.
Kutokana na kauli hiyo, Katibu Mkuu wa CCM
alisema huo ni uzushi wa hali ya juu na kuitaka halmashauri hiyo kuacha mara
moja tabia ya kuwaonea walimu kwa kusingizia viongozi mambo mabaya ya fitina.
“Kuanzia sasa CCM imeamua kuingia kati
kufuatilia matatizo ya walimu yakiwamo madai yao na kwa kweli itahakikisha
yanalipwa” alisema.
Awali akihutubia mkutano wa hadhara kwenye
Uwanja wa Baraza la Kata, Kinana aliwasihi Watanzania kuendelea kuiamini
Serikali ya CCM akisisitiza inalenga kuwatetea wanyonge na kuboresha maisha.