Na Elisante John, Singida
Januari 16, 2014:WATU 12 akiwemo diwani wa kata ya Unyambwa
(CCM) Manispaa ya Singida Shabani Satu (47), wamefikishwa mahakamani mjini
Singida jana Ijumaa, kwa shitaka la kuchoma moto basi la Mtei Express, wakati
likiwa safarini kutoka Singida Mjini kwenda Mkoani Arusha.
Wengine walioshitakiwa pamoja na diwani huyo ni Salumu Shabani
(20), Hashimu Hamisi (20), Hasani Itambu (54), Ahmed Abdarlahaman (24), Shabani
Hamisi (29) na Japhet Eliakimu (38) wote wakazi wa Kisasida, katika Manispaa ya
Singida.
Pia katika shitaka hilo wapo washitakiwa wengine 11 ambao ni
Shamushadini Adamu (32), Ally Jafari (19), Ali Mohammed (29) na Yasini Emmanuel
(23) wote wakazi wa Unyambwa katika Manispaa ya Singida na Michael Andrew (30)
mkazi wa Unyankhae, Singida vijijini.
Mbele ya hakimu wa mahakama ya hakimu mkazi mjini Singida Asha
Mwetindwa, ilidaiwa na mwendesha mashitaka wa polisi Musa Chemu kuwa
washitakiwa walifanya kosa hilo Januari tisa mwaka huu, saa 1:30 asubuhi katika
Kijiji cha Kisasida, kata Unyambwa tarafa ya Mungumaji, Manispaa ya Singida.
Chemu alisema kuwa, washitakiwa kwa pamoja wakiwa na nia ovu,
walilichoma kwa moto basi la kampuni ya Mtei Express, lenye namba za usajili T
742 ACU Scania, lenye thamani ya Sh. Milioni 70 na kusababisha hasara na
uharibifu mkubwa.
Mwendesha mashitaka katika kesi hiyo aliieleza mahakama hiyo
kuwa, upelelezi zaidi wa shauri hilo bado unaendelea na kesi hiyo limepangiwa
hadi Januari 30 mwaka huu.
Hakimu Mwentindwa aliwaeleza washitakiwa kuwa dhamana ipo wazi
kwa kila mmoja kuwa na wadhamini wawili, wenye mali isiyohamishika kwa kila
mdhamini awe na thamani ya Sh. Milioni 35, huku mali hizo ziwe zimefanyiwa
tathimini na mamlaka husika katika Manispaa ya Singida.
Hata hivyo washitakiwa wote walikana kosa hilo na hadi NIPASHE
inaondoka mahakamani hapo saa tano mchana, hakuna mshitakiwa
aliyekuwa ametimiza masharti ya dhamana, hivyo kulazimika kurejeshwa tena
mahababusu.
MWISHO.