Bw. McDonald Maganga, Meneja wa SIDO Kigoma |
Maonesho ya bidhaa zinazozalishwa na viwanda vidogovidogo
kanda ya kati yamemalizika kwa mafanikio makubwa mjini Kigoma nchini Tanzania huku yakiacha
changamoto kadhaa za mitaji na masoko ya bidhaa husika.
Washiriki wa maonesho hayo kutoka mikoa ya Dodoma, Singida,
Tabora na mwenyeji Kigoma wamekiri kuwepo kwa matatizo ya mitaji pamoja na
ukosefu wa soko la uhakika ndani na nje ya nchi, jambo linalodhoofisha wamiliki
wa viwanda na wajasiriamali.
Sehemu ya Mabanda yaliyotumika katika maonesho ya biashara maarufu kama maonesho ya SIDO Kigoma |
Wakiongea na mtandao huu katika kilele cha maonesho hayo wameomba serikali na taaisisi zake kuwawezesha
wajasiliamali kupata mitaji kwa njia ya mikopo yenye riba nafuu pamoja fursa za
masoko.
Mmoja wa washiriki wa maonesho hayo Bi. Cotrida Kokupima
kutoka wilayani Kasulu Mkoani Kigoma, amesema licha ya serikali kuwa na sera nzuri za kusaidia wajasiriamali bado
taasisi za fedha hasa Benki hazijatoa unafuu kwao.
Naye Bw.Hamis Rudonongo kutoka Dodoma amesema watumishi wa
umma katika kada ya chini, wanakiuka maadili ya utumishi wao kwa kuwanyima
huduma wajasiriamali wadogo.
Kwa upande wake meneja wa shirika la
maendeleo ya viwanda vidogo SIDO mkoani Kigoma Bw. McDonald Magnaga ambaye ndiye alikuwa
mwenyeji wa maonesho hayo amesema licha ya changamoto zinazotajwa na wadau,
maonesho hayo ya mwaka yamekuwa ufunguo wa fursa za masoko
Licha ya kukiri kuwepo kwa tatizo la soko la nje ya Tanzania,
McDonald amebainisha kuwa SIDO inao mfuko maalumu kwa kuwakopesha Mitaji wajasiriamali
wanaotimiza vigezo.
Bw. McDonald Maganga amebainisha kuwa Shirika hilo la viwanda
vidogo linazo fursa za mikopo ambapo waasiriamali hukopeshwa kati ya sh.
milioni mbili hadi sita.
Zaidi ya wajasiriamali 270 kutoka mikoa ya kanda ya kati pamoja
na nchini Kenya wameshiriki maonesho hayo.
Kwa mujibu wa taarifa za SIDO kiasi cha zaidi ya shilingi
milioni mia mbili kimekopeshwa kwa wajasiriamali wadogowadogo katika kipindi
cha mwaka 2013/2014