Kanali Issa Machibya, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma |
Kutokana na kuwa jirani na nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya
Congo, ambayo imeripotiwa kuwa na wagonjwa wanaodhaniwa kuugua Ebola, mkoa wa
Kigoma umeanza kuchukua tahadhari kuzuia ugonjwa huo usiingie Tanzania
Mkuu wa mkoa wa Kigoma kanali mstaafu Issa Machibya
amebainisha hayo wakati akitoa taarifa kwa waandishi wa habari kuhusu hofu na
tahadhari hiyo baada ya serikali ya DRC na shirika la afya duniani WHO kukiri
kuwa raia kadhaa wa DRC walioambukizwa virusi vya Ebola.
Kanali machibya amebainisha kuwa kutoka katika eneo
linalohofiwa kuibuka kwa ebola nchini DRC hadi mkoani nchini Tanzania eneo la
mkoa wa Kigoma ni kiasi cha kilomita arobaini na tano pekee upande wa ziwa
Tanganyika.
Aidha amezitaka mamlaka za afya Kinga pamoja na idara za
uhamiaji kushirikiana kuhakikisha wageni wanaoingia nchini Tanzania kutoka DRC
, Burundi na Zambia kuchunguzwa kwa umakini na atakayetiliwa shaka hatua za
haraka zichukuliwe ili kuepuka maambukizi nchini Tanzania.
Naye katibu tawala mkoa wa Kigoma mhandishi John Ndunguru
amesisitiza kuwa, mkoa kwa kushirikiana na idara ya afya umeanza kutoa elimu wa
wananchi
Pamoja na maagizo hayo wananchi wanaofanya shughuli za uvuvi
na biashara katika bandari ndogo za Kibirizi na Ujiji mkoani Kigoma wameikosoa
serikali kwa kutotoa mafunzo ya kutambua dalili za ebora pamoja na namna ya
kujikinga na maambukizi.
Katibu wa chama cha wavuvi na wamiliki wa mitumbwi mkoa wa
Kigoma Bw. Muhamed Kasambo ameeleza kuwa, bandari ndogo hizo hupokea wageni
kutoka DRC na Burundi kila siku na serikali haijaweka kituo cha afya ili
kuwachunguza wageni hao
Kwa upande wake Bw. MPOROGOMYI SALUM Ambaye ni mvuvi na
msafirishaji wa bidhaa za ziwa Tanganyika kutoka Kigoma kwenda Burundi, DRC na
Zambia amesema serikali ya Tanzania inapaswa kutoa elimu kwa wananchi wake
hususani wasafirishaji katika ziwa Tanganyika ili wafahamu dalili na namna ya
kujikinga na ebola.
Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wetu katika mwalo wa Kibirizi na Ujiji hakuna matangazo yaliyofafikia wavuvi wala vipeperushi kuhusu tahadhari ya Ebola, licha ya mkuu wa mkoa wa Kigoma kanali Machibya kuagiza matangazo kufanyika.