Home » » MWANAMKE SHUJAA ALIYEPAMBANA KIVITA NA WAKOLONI WA UTAWALA WA KIJERUMANI

MWANAMKE SHUJAA ALIYEPAMBANA KIVITA NA WAKOLONI WA UTAWALA WA KIJERUMANI

Written By Unknown on Jumanne, 3 Septemba 2013 | 09:18

Na Daud Nkuki – Singida
Mwanamke shujaa aliyewaongoza kabila la Wanyaturu katika mapambano dhidi ya utawala wa kijerumani, si mwingine ila ni Leti Kidanka, katika vita vikuu vya pili vya dunia mwaka 1938 hadi 1945.
Kwa mujibu wa familia iliyopo, Leti alizaliwa katika kijiji cha Unyang’ombe – Sekotoure Ilongero. Aliolewa na Nyalandu Mtinangi wa Ukoo wa Lundi (antuamwa Lundi). Katika kijiji cha Matumbo Kitongoji Mikuyu, Kata ya Makuro wilayani Singida vijijini.
Wazazi wake walikuwa waganga wa tiba asilia Kidanka Jilu Msasu na Sita Mughenyi,  Leti naye alirithi uganga huo toka kwa wazazi wake.
Ushujaa wake ulijitokeza zaidi katika ukoo mdogo wa Lundi alikoolewa. Wakati alipowatumia nyuki kama silaha ya kudhoofisha nguvu za maadui wake na kuwasambaratisha walipojaribu kumkaribia.
Maadui wake wakuu, walikuwa ni wakoloni wa Kijerumani wakishirikiana na vibaraka wao wa ukoo wa Unyanjoka ukiongozwa na Igwe Yunga kumkabili mwanamke huyo.
Mapambano hayo yalichukua miaka mitatu 1908 hadi 1910. Kibaraka Igwe alitafuta nguvu za ziada za kukabiliana na Leti alipolileta jeshi la kijerumani kutoka kilimatinde wilayani Manyoni, baada ya wao kushindwa.
Katika pambano hilo la mara ya pili kati ya wajerumani Wanyanjoka na kikosi cha Leti. Wakati askari wa kijerumani aliyejulikana kwa jina moja la “SAUSI” aliuwawa kwa kuchomwa mkuki na mume wa shujaa huyo Nyalandu Mtinangi mwaka 1909.
Leti alipambana na maadui hao mara mbili na kuwashinda. Safari ya tatu mnamo mwaka 1910 hakuweza kufanikiwa kuwashinda, badala yake aliuwawa nyumbani kwake pamoja na mume wake katika kijiji cha Matumbo Kitongoji cha Mikuyu Singida vijijini.
Umaarufu wa Leti ulitokana na ujasiri aliokuwa nao akiwa ni mwanamke, kwa kuwatumia nyuki kama silaha yake ya kuwashambulia maadui huku akisaidiwa na wafuasi wake ambao walikuwa ni mume wake Nyalandu na shemeji yake Hango Linja, wakitumia Mikuki na mishale.
Mwanamke huyo aliongoza mapambano yeye mwenyewe kwa kutoa amri kwa washirika wake kushambulia au kusitisha mapigano katika eneo la vita.
Aidha alijihami kwa kutumia (sumanda) handaki kujificha wasionekane kwa maadui. Hivyo ni baadhi ya vitu vilivyo mjengea umaarufu wa kujulikana katika historia ya mapambano dhidi ya wajerumani.
Kuanguka kwake ni pale dawa zake zilipokosa nguvu, hatimaye kuuwawa, baada ya kusababishwa na mwenzake waliokuwa shirika moja, Sie Ndida mke wa shemeji yake Hango Linja, walioishi eneo moja kujenga urafiki na Igwe Yunga uliomfanya atoe siri ya ushujaa wao.
Sie alirudi kwa siri kwenye eneo la zindiko, bila mwenzake kujua alihamisha dawa zote upande wake. Mwenzake Leti alipojaribu kutumia dawa zake alipowaona adui zake wanakaribia zilishindwa kufanya kazi. Matokeo yake alikutwa nyumbani akijikalia na kupigwa risasi wakiwa na mume wake na kufariki pale pale. Miili yao ilizikwa baada ya siku tatu, watu wakihofia kurudi tena adui zao.
Hapo ukawa mwisho wa mapambano, hawakuendelea kwenda kwa Sie kwa kuwa aliwaonyesha siri ya ushujaa wao. Ukweli huo unadhihirishwa na wimbo wa kinyaturi usemao, “Sie Sie na Leti, asunguatufu, vikhoma Nkingi Vasuka vikuranga …”(maana yake walikuwa wakiimba Sie, Sie na Leti wanawake watupu mamezipiga mambo na kuzingoa mwenyewe).
Leti alikuwa na watoto wanne, wawili wa kiume na wengine wa kike. Kati ya yao watatu moja wa kiume aliitwa  Sang’ida, wasichana ni Nyamughenyi na Sita walikamatwa na kuchukuliwa na wajerumani kupelekwa Dar es salaam, baada ya wazazi wao kuuwawa. Licha ya kuwachukua watoto hao pia walichukua kichwa cha mama yao hadi Ujerumani.
Mtoto mwingine aliyeitwa Kidanka, katika purukushani hizo, aliweza kuwatoroka akiwa na jeraha la risasi ubavuni mwake. Kwa kuwa walikuwa na asili ya uganga, naye alipona na kuendelea na shughuli hiyo mpaka alipofariki mwaka 1980 kijijini hapo.
Mpaka sasa koo hizi mbili Lundi na Unyang’ombe hushirikiana kutambika mara kwa mara, katika eneo husika yalipo makaburi ya watu hao, kwa nia ya kunusuru majanga yanayoweza kutokea.
Familia, jamii inaungana na wazee mkoani Singida, katika risala yao kwa Mkuu wa Mkoa mwaka jana, walipokuwa wakiadhimisha siku ya wazee duniani kuiomba serikali ilipe kupaumbele swala la kurejesha nchini fuvu la kichwa cha shujaa huyu, kama ilivyofanya kwa chifu Mkwawa.
Mwisho.
Share this article :
 
Shukrani kwa : Harold Dickson | Prosper Kwigize | 0752490120
Copyright © 2013. KWIGIZE NEWS AND COMMUNICATION - Haki zote zimeifadhiwa
Email us: kwigizenews@gmail.com
0764243377