Eneo la mpaka wa Tanzania na Burundi, Manyovu wilayani Buhigwe mkoani Kigoma |
WATU wanne wamepoteza maisha na wengine watano
wamejeruhiwa kufuatia bomu la kurusha kwa mkono lililotupwa kwenye gari la
abiria na watu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi kutoka nchi jirani ya Burundi.
Habari zilizopatikana kutoka eneo la
tukio na baadaye kuthibitishwa na Mwenyekiti wa serikali ya kijiji cha Kilelema,
Benedict Samson zinaeleza kuwa tukio hilo limetokea mapema jana asubuhi kati ya
kijiji cha Kilelema na Migongo wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma.
Mwenyekiti huyo amesema kuwa alipata
taarifa za kuwepo kwa tukio majira ya asubuhi na baadaye kwenda eneo la tukio
ambapo anasema kuwa katika tukio hilo watu watatu ambao wanasadikiwa kuuawa
huku wengine sita wakijeruhiwa miongoni mwao wawili wakijeruhiwa vibaya.
Alisema kuwa baada ya kuenea kwa
habari hizo muda mchache baadaye waliwasili wanajeshi kutoka katika vikosi
vilivyopo maeneo ya mpakani ambao walitoa msaada wa dharula na baadaye
kuwachukua maiti na majeruhi na kuwapeleka hospitali ya wilaya ya Kasulu kwa
matibabu ya dharula.
Kwa upande wake,Augustino Mkuvata
Mwalim katika shule ya Msingi Kilelema ambaye alikuwa mmoja wa abiria kwenye
gari aina ya Toyota Hiace waliyokuwa wakisafiria anasema kuwa kabla ya bomu
kurushwa kwenye gari awali walisimamishwa na mtu aliyesimama kati kati ya
barabara akiwa na bunduki.
Mkuvata alisema kuwa baada ya mtu
huyo kusimamisha gari dreva alibaini kwamba mtu huyo anaweza kuwa jambazi na
kwamba badala ya kusimamia na kwa kuwa kulikuwa hakujapambazuka aliwasha taa na
kuzizima jambo lililomchanganya jambazi huyo na kusogea pembeni ambapo dereva
aliongeza mwendo ili kukimbia.
Akisimulia tukio Mwalim kuvata
alisema kuwa baada ya kitendo hicho abiria walilala chini ya viti vya gari
wakihofia kupigwa risasi lakini alijitikeza mtu mwingine mbele ya gari na
kurusha bomu ambalo lililipua gari hilo.
Mkuu wa polisi wilaya ya
Buhigwe,Frank Utonga amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kwamba kwa
sasa wako eneo la tukio wakishughulikia jambo hilo na kwamba taarifa ya nini
kimetokea zitatolewa baadaye.
Kamanda wa polisi mkoa Kigoma,
Jafari Mohamed hakuweza kupatikana kuzungumzia tukio hilo kwa kile
kilichoelezwa na wasaidizi kwake ameelekea eneo la tukio.