Jeshi la Polisi Mkoani Kigoma linawashikilia watu wanne kwa
tuhuma za kuchoma moto Masijala ya Idara ya Ardhi ya Manispaa ya Kigoma Ujiji
na kuteketeza Hati na Nyaraka mbali mbali za idara hiyo
Kamanda wa Polisi Mkoani Kigoma, ACP Jafari Mohamed amethibitisha
kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa wanaoshikiliwa watafikishwa mahakamani
baada ya uchunguzi kukamilika.
Kamanda Mohamed amewataja watu hao kuwa ni Anna Fanuel (46),
mhudumu wa ofisi, Makrina Paul (49),Karani, Saimon Pius (37),mkazi wa Burega na
Tumaini Esau (44), mkazi wa Mwasenga, Manispaa ya Kigoma Ujiji.
Alisema kuwa mnamo Octoba mosi mwaka huu majira ya saa nne na
robo usiku Masijala ya Idara ya Ardhi ya Manispaa ya Kigoma Ujiji ilichomwa
moto na kuteketeza hati na nyaraka mbali mbali kitendo ambacho ni kinyume cha
Sheria.
Inadaiwa kuwa kitendo hicho ni njama ya kupoteza vielelezo
nyeti kutokana Idara hiyo kughubikwa na migogoro inayohusiana na ugawaji wa
viwanja.
Kamanda Mohamed alisema mbinu iliyotumika ni kuchoma ofisi
kwa kutumia mafuta ya Petroli.