 |
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. John Pombe Magufuli |
Mheshimiwa Spika;
Niko hapa leo kutimiza matakwa ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Ibara ya 91 Ibara ndogo ya kwanza inayonitaka kulihutubia na kulifungua rasmi
Bunge hili. Naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia uzima na afya njema,
na kutuwezesha kuwepo hapa siku ya leo.
Aidha nitumie fursa hii kuwakumbuka wenzetu ambao, kwa namna na nafasi
mbalimbali, walishiriki katika mchakato wa uchaguzi huu na kwa bahati mbaya
walipoteza maisha yao kabla ya mchakato haujakamilika. Kwa hao wote
waliotangulia mbele za haki ninamuomba Mwenyezi Mungu azirehemu roho zao na
awape pumziko la amani. Nitumie nafasi hii kuwapa pole ndugu na jamaa ambao
ndugu zao walifariki na wengine kupata ulemavu wakati wa mchakato wa uchaguzi
huu.
Pia natoa pongezi kwako wewe Mheshimiwa Spika, Job Ndugai na Mheshimiwa Naibu
Spika, Dkt. Ackson Tulia kwa kuchaguliwa kwenu kuongoza Bunge letu la 11.
Waheshimiwa Wabunge wamewapa imani yao, na mimi kwa nafasi yangu nawahakikishia
imani na matumaini yangu makubwa kwenu. Sina shaka Mheshimiwa Spika, chini ya
uongozi wako Bunge letu limepata kiongozi mahiri, makini na mweledi.
Aidha, niwapongeze Wabunge wote kwa kuchaguliwa kuwa wabunge wa Bunge hili la
11. Aidha, nitumie nafasi hii kuwapongeza wale wote waliochaguliwa katika
nafasi za udiwani katika kata mbalimbali kote nchini. Natoa pongezi hizi kwa
dhati kabisa kabisa kwa sababu kuu mbili:
- Kwanza,
ni kwa sababu ushindani katika uchaguzi wa mwaka huu ulikuwa ni mkubwa
sana kuanzia ndani ya vyama vyetu na baadae katika Uchaguzi Mkuu
uliohusisha na kushindanisha wagombea toka vyama tofauti.
- Pili,
nawapongeza kwa sababu wananchi wamewapa imani na ridhaa ya kuwawakilisha
katika kipindi ambacho matarajio yao kwa Awamu ya Tano ya uongozi wa nchi
yetu ni makubwa sana. Watatupima kwa namna tutakavyokidhi kiu na matarajio
yao. Sote tuliahidi kuwatumikia wananchi, na kutokana na utumishi wetu
kwao tuweze kutatua matatizo yao mbalimbali, na kuongoza mabadiliko
makubwa ya kiutendaji, usimamizi wa matumizi ya mali za umma na rasilimali
za taifa, na ugawaji wa rasilimali hizo kwa haki.
Mimi na Mheshimiwa Samia Suluhu, Makamu wa Rais tuliwaahidi wananchi kuwa
tutawatumikia na tutahakikisha kuwa katika utumishi wetu tutawajali wananchi
wote, lakini zaidi wananchi wa kawaida. Naamini wenzangu pia ndicho mlichoahidi
na daima tukumbuke kuwa kazi zetu na mipango yetu yote tutakayoipanga na
kuisimamia italenga katika kuwanufaisha watu wetu.
Mheshimiwa Spika;
Niwahakikishie tu wananchi kuwa mambo tuliyowaahidi tutayatekeleza. Sikusudii
kurejea mambo yote niliyoahidi katika hotuba yangu hii ya leo, lakini nataka
niwatoe wasiwasi kabisa kwamba tuliyoahidi tumeahidi na ahadi ni deni. Nataka
Wananchi mniamini kuwa sikutoa ahadi ili tu mnipigie kura, niliahidi
kuwatumikia na kuwafanyia kazi, na hicho ndicho nitakachofanya. Ni imani yangu
kwamba Waheshimiwa Wabunge na Madiwani pia watafanya hivyo hivyo kama
tutakavyofanya sisi.
Napenda pia kutoa shukrani zangu za dhati kabisa kwa Watanzania wote.
Tulijiandikisha kwa wingi sana kwa ajili ya kupiga kura, tulishiriki na kufuatilia
kwa karibu sana kampeni za uchaguzi, na tukajitokeza kwa wingi siku ya kupiga
kura. Kinyume na ilivyotabiriwa na wasio tutakia mema hakuna siku iliyokuwa na
utulivu mkubwa na amani kama siku ya tarehe 25 Oktoba tulivyokwenda kupiga
kura. Hata baada ya matokeo kuanza kutangazwa tulionyesha utulivu mkubwa, na
hata pale ambapo matokeo yalipotangazwa na yakawa sivyo baadhi yetu
walivyoyatarajia bado tuliyapokea kwa hali ya utulivu na uungwana mkubwa.
Wale waliotarajia kuwa tutafarakana wameondoka wakiwa wamefadhaika sana huku
wakijiuliza hivi hawa Watanzania ni Waafrika wa namna gani. Ndugu zangu
Watanzania, kwa mara nyingine tena tumedhihirisha, kwetu sisi wenyewe, kwa
Afrika na dunia, kwamba sisi ni kisiwa cha Amani katika bahari iliyochafuka.
Tunayo haja ya kujipongeza na kujiwekea nadhiri kuwa tuaendelea kuidumisha hali
hii na kuilinda amani ya nchi yetu. Ombi langu kwa vyama vya siasa, wanasiasa
wa vyama vyote na viongozi wa dini ni kutimiza wajibu wetu wa kuilea amani ya
nchi yetu.
Aidha, napenda niungane na ninyi pamoja na Watanzania wote kuvipongeza vyombo
vyetu vya Ulinzi na Usalama (Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), Polisi,
Magereza, Uhamiaji na Usalama wa Taifa pamoja na mgambo) kwa jinsi
walivyoshiriki katika kuhakikisha nchi yetu inaendelea kuwa salama katika
kipindi chote cha uchaguzi.
Nawapongeza pia Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa namna walivyosimamia zoezi zima
la uchaguzi toka hatua za awali za kujiandikisha hadi siku ya kupiga kura na
kutangaza matokeo. Mmetimiza wajibu wenu kwa weledi na umahiri mkubwa katika
mazingira magumu na yenye changamoto nyingi. Hongereni, hongereni sana!
Mheshimiwa Spika;
Naomba kwa namna ya pekee, niwashukuru viongozi wakuu wa nchi yetu
walionitangulia kwa kazi kubwa na nzuri walioifanyia nchi yetu. Natambua
mchango wa Waasisi wa taifa letu, Mwalimu Nyerere na Mzee Karume kwa kujenga
misingi imara wa umoja, mshikamano na amani ya nchi yetu. Mzee Mwinyi (Mzee
Ruksa) kwa kuleta mabadiliko ya kiuchumi na kisiasa na kuijenga misingi yake.
Mzee Mkapa (Mzee wa Ukweli na Uwazi) kwa kupanua na kuimarisha misingi ya
uchumi na siasa ya nchi yetu. Mzee Kikwete (Mzee wa Maisha Bora) kwa kuendeleza
misingi hiyo na kupanua fursa mbalimbali kwa wananchi kujiletea maendeleo yao.
Wamefanya kazi kubwa. Nawashukuru sana na ninawatakia uzee mwema na maisha
marefu ili tuzidi kuchuma busara zao.
Mhishimiwa Spika;
Tumeingia kwenye uchaguzi wamoja, tumeshindana katika kampeni tukiwa wamoja, na
tumemaliza uchaguzi wetu tukiwa wamoja. Nataka niwahakikishie Waheshimiwa
Wabunge na Watanzania kwa ujumla kwamba Serikali ya Awamu ya Tano itaendelea
kulinda kwa nguvu na uwezo wote Tunu hizi za Umoja na Amani. Hatutakuwa na
simile kwa mtu au kikundi chochote ambacho kitataka kuvuruga umoja na amani
yetu kwa misingi ya udini, rangi, ukabila, vyama au ukanda.
Mheshimiwa Spika;
Wakati wa kampeni, yako maeneo yaliyojitokeza kwa kulalamikiwa sana na
wananchi. Ningependa niyataje baadhi ya maeneo yaliyolalamikiwa, maeneo hayo ni
pamoja na:
- Rushwa -
Suala la rushwa limelalamikiwa sana takriban katika maeneo yote yanayogusa
wananchi.
- TAMISEMI
- Upotevu wa mapato, kushindwa kukusanya kodi, ubadhirifu, matumizi mabaya
ya fedha na utekelezaji wa baadhi ya miradi chini ya viwango, wizi,
uzembe, n.k.;
- Ardhi -
Migogoro ya wakulima na wafugaji, viwanja, kuhodhi maeneo bila
kuyaendeleza, mipango miji, kujenga maeneo ya wazi, n.k.;
- Bandari
- Rushwa, wizi, ubadhirifu na urasimu;
- Maji -
Kiwango cha chini cha upatikanaji wa maji safi na salama, huduma ya maji
kupatikana mbali na makazi, n.k.;
- TRA -
Ukwepaji kodi, rushwa, ubadhirifu, urasimu na upotevu wa mapato kwa
kushindwa kukusanya kodi hasa kodi zinazotakiwa kulipwa na wafanyabishara
wakubwa;
- TANESCO
- Kukatika kwa umeme mara kwa mara na uwepo wa umeme wa mgao;
- Maliasili na Utalii
- Ujangili ambao lazima Idara husika inashiriki, Migogoro ya mipaka kati
ya vijiji na Hifadhi, Upotevu wa mapato, n.k.;
- Huduma za Afya (Hospitali) - Huduma kuwa mbali na wahitaji, Ukosefu wa madawa,
hujuma kwenye vifaa vya vipimo, msongamano wa wagonjwa na tozo
zisizostahili, lugha mbaya za watumishi kwa wagonjwa, uhaba wa majengo,
vitendea kazi, rasilimali watu na fedha, kushindwa kukusanya mapato
yanayowahusu, n.k.;
- Uhamiaji na Ajira
- Kutoa hovyo hati za uraia, Vibali vya kuishi nchini kwa wageni,
Kushindwa kusimamia ajira za wageni hususan kwa kazi zinazoweza kufanywa
na wazawa, n.k.;
- Elimu
- Uhaba wa vifaa vya kujifunzia na kufundishia, michango mingi isiyo ya
lazima, malalamiko ya walimu yasiyoisha, mazingira ya kusomea ikiwa ni
pamoja na majengo, Madawati, Ukosefu wa nyumba za walimu, n.k.;
- Polisi -
Malalamiko ya wananchi kubambikiwa kesi, upendeleo, Madai ya askari,
Ukosefu wa nyumba za askari, Ukosefu wa vitendea kazi vya kisasa, n.k.;
- Zimamoto
- Kuchelewa kufika kwenye matukio, kufika kwenye matukio bila vitendea
kazi kama maji, n.k.;
- Mizani -
kucheleweshwa kwa magari yanayosafiri;
- Mahakama -
Natambua jitihada za Mahakama katika kushughulikia swala la mrundikano wa
kesi. Hata hivyo, bado kumekuwa na malalamiko mengi juu ya ucheleweshaji
wa kesi.
- Madini -
Wenyeji kutofaidika, Vilio vya wachimbaji wadogowadogo kutengewa maeneo ya
uchimbaji na kupatiwa mikopo, kutolipa kodi stahiki, usumbufu kulipa
fidia, n.k;
- Kilimo na Mifugo ?
Uhaba wa pembejeo za mifugo na kilimo, Tatizo la masoko, Kukopwa mazao ya
wakulima, Ukosefu wa Wataalamu wa Ugani, Upungufu wa Maghala, Mabwawa,
Malambo, Majosho, n.k.;
- Uvuvi -
Vifaa duni na masoko, Uvuvi haramu, Uwekezaji mdogo katika Sekta ya Uvuvi
hususan viwanda vya mazao ya uvuvi n.k., na hasa katika ukanda wetu wa
bahari;
- Reli -
Uchakavu wa miundombinu ya nchi, Kutokuwepo kwa usafiri wa uhakika wa
reli, upungufu wa bandari kavu, Mizigo mingi kusafirishwa kwa barabara,
n.k.;
- ATC -
Shirika la Ndege lipo, Wafanyakazi wapo zaidi ya 200, na wanalipwa
mishahara ila ndege ni moja (1);
- Makundi Maalum -
Haki za wazee, Walemavu, Wanawake na watoto zimekuwa zikikiukwa;
- Wafanyakazi, Wasanii na Wanamichezo ? Mzigo wa kodi kwa wafanyakazi, Haki na maslahi yao,
n.k.;
Kero hizi tutazishughulikia kwa nguvu zetu zote. Wizara, Ofisi na Taasisi
husika zijipange ipasavyo kutatua kero hizi. Nimetaja baadhi ya kero hizi ili
nanyi Waheshimiwa Wabunge mzitambue na mshirikiane na Serikali na wadau wengine
tuzitatue haraka.
Pamoja na kero hizo tutashughulikia pia mambo yafuatayo.
Kuimarisha Muungano
Mheshimiwa Spika;
Nilipoapa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, niliapa kuulinda
Muungano wa nchi yetu. Hata bila kiapo, mimi ni muumini wa dhati wa Muungano
wetu wa kipekee, uliounganisha nchi mbili zilizokuwa huru za Jamhuri ya
Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar, tena kwa hiari na kwa wino wa
kalamu, na si mtutu kama miungano mingine duniani.
Naamini kwa dhati ya moyo wangu kuwa Muungano wetu ndio umoja wetu, amani yetu
na salama yetu. Ninayo kila sababu ya kuulinda na kuuenzi Muungano wetu adhimu
na adimu. Ni azma yangu kuwaona wananchi wa Zanzibar na Bara wakifurahia
matunda ya Muungano wetu badala ya kuwa kikwazo kwa ustawi wao na ustawi wa
nchi yetu.
Aidha, kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na wadau wa siasa
hususan vyama vya CUF na CCM tutahakikisha kuwa majaribu ya kisiasa
yanayoikabili Zanzibar yanamalizika kwa salama na amani. Tunamuomba Mwenyezi
Mungu atujalie busara na hekima tumalize kwa utulivu na amani.
Serikali nitakayoiunda itafanya kila lililo ndani ya uwezo wake kuendelea
kuimarisha Muungano wetu. Nina faraja kuwa Mheshimiwa Samia Suluhu, Makamu wa
Rais anao uzoefu mkubwa kutokana na nafasi yake ya awali ya Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia Muungano, na pia akiwa Makamu
Mwenyekiti wa Bunge la Katiba. Mimi pamoja na Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu
na Rais wa Zanzibar, Dkt. Ali Mohamed Shein tutahakikisha tunasimamia na
kuimarisha Muungano wetu.
Kuimarisha Mihimili ya Serikali
Mheshimiwa Spika;
Serikali ya Awamu ya Tano itaheshimu na kuendeleza utamaduni mzuri uliojengeka
nchini wa kuheshimu mihimili ya dola. Tutafanya hivyo kwa kuhakikisha kuwa
mihimili yetu ya Bunge na Mahakama inapata fedha za kutosha kuendesha
shughuli zake kwa uhuru kupitia Mfuko wa Bunge na Mfuko wa Mahakama. Kwa upande
wa Bunge, tutahakikisha fedha za Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo zinapatikana kwa
wakati ili Waheshimiwa Wabunge mkashirikiane na wananchi wenu kusukuma
maendeleo. Kwa upande wa Mahakama, tutalipa uzito mkubwa suala la uboreshaji wa
Mahakama kwa kusogeza huduma za Mahakama karibu na wananchi, kuongeza kasi ya
utoaji haki na kuboresha maslahi ya watumishi wa Mahakama zetu.
Mchakato wa Katiba
Mheshimiwa Spika;
Serikali yangu imepokea kiporo cha mchakato wa Katiba ambao haukuweza
kukamilika katika Awamu iliyopita kutokana na kutokukamilika kwa wakati kwa
zoezi la uandikishaji wapiga kura. Napenda kuwahakikishia kuwa tunatambua na
kuthamini kazi kubwa ya kizalendo iliyofanywa na wananchi walioshiriki hatua ya
awali ya ukusanyaji wa maoni kuhusu Katiba mpya, Tume ya Marekebisho ya Katiba
na Bunge la Katiba lililotupatia Katiba Inayopendekezwa. Tutatekeleza wajibu
wetu kama ulivyoainishwa katika Sheria ya Marekebisho ya Katiba.
Uchumi na Matarajio ya Wananchi
Mheshimiwa Spika;
Serikali ya Awamu ya Tano inaingia madarakani kukiwa na msingi imara wa
kiuchumi uliojengwa katika Awamu inayomaliza muda wake. Uchumi wa nchi yetu
umekuwa ukiimarika na kukua wastani wa asilimia 7. Katika kipindi hicho
fursa mbalimbali za kiuchumi zilizopo nchini mwetu zimezidi kufunguliwa. Hii ni
kutokana na jitihada zilizofanywa na Serikali za Awamu zilizopita za kujenga
miundombinu ya kiuchumi kama vile barabara, uimarishaji wa bandari, uimarishaji
wa reli, na ukuzaji wa sekta za mawasiliano ya simu na mitandao, ukuzaji na
uongezaji wa uwezo wetu wa kuzalisha na kusambaza umeme.
Napenda kuwahakikishia kuwa tutaendeleza na kuimarisha ujenzi wa miundombinu
mipya na kuiimarisha iliyopo ili kuvutia na kushawishi wawekezaji wa ndani na
wa nje.
Mheshimiwa Spika;
Nasema hivi kwa sababu miongoni mwa ahadi tulizowaahidi Watanzania ni
kuendeleza ujenzi wa barabara mbalimbali za kuunganisha miji yetu mikuu ya
mikoa na wilaya; barabara ziendazo kwenye maeneo muhimu ya kimkakati na
kiuchumi; na upanuaji wa barabara za miji kama Dar es Salaam kwa kujenga flyovers,
barabara za pete (ring roads), n.k. Uboreshaji wa barabara na njia
nyingine za uchukuzi na usafirishaji kuingia na kutoka Dar es Salaam ni muhimu
sana kwa sababu bandari ya Dar es salaam ni lango kuu la biashara kwa nchi yetu
na nchi jirani.
Mheshimiwa Spika;
Katika jitihada hizo hizo za kuboresha na kuimarisha miundombinu ya kiuchumi
Serikali ya Awamu ya Tano, katika kipindi cha miaka mitano ijayo itaelekeza
nguvu zake katika ujenzi wa reli mpya katika kiwango cha kimataifa (yaani
standard gauge). Reli ambazo tunakusudia zianze kujengwa ni:
- Dar es Salaam - Tabora - Kigoma/Mwanza
- Uvinza - Msongati (Burundi) na Isaka - Kigali (Rwanda)
- Mtwara - Songea - Mbamba Bay na matawi ya kwenda
Mchuchuma na Liganga;
- Tanga - Arusha - Musoma
- Kaliua - Mpanda - Karema
Mheshimiwa Spika;
Nchi yetu pia imejaliwa kuwa na madini na maliasili nyingi. Ugunduzi wa gesi
asilia umeongeza matumaini ya watu wetu wengi juu ya uwezo wetu wa kiuchumi
katika miaka ijayo. Serikali itahakikisha kwamba madini na maliasili zetu
zinatumika kwa manufaa ya Taifa letu kwa kusimamia Sheria na Taratibu zilizopo.
Aidha, napenda kuipongeza kwa dhati kabisa Serikali ya Rais Jakaya Mrisho
Kikwete na Bunge la 10 kwa kupitisha Sheria ya Usimamizi wa Mapato ya Mafuta na
Gesi yaani The Oil and Gas Revenues Management Act, 2015.
Serikali yangu itasimamia utekelezaji wa sheria hiyo kwa uaminifu na umakini
mkubwa.
Ujenzi wa Viwanda
Mheshimiwa Spika;
Serikali ya Awamu ya Tano itaweka mkazo mkubwa katika ujenzi wa Viwanda.
Natambua kwamba sekta binafsi ndiyo muhimili mkubwa wa kujenga uchumi wa
viwanda. Hatuna njia nyingine kama kweli tunataka kujenga msingi wa uchumi
endelevu katika nchi yetu utakaopaisha uchumi na maisha ya watu wetu. Dira ya
Maendeleo ya 2025 inatutaka tuwe nchi ya watu wenye kipato cha kati.
Tunaweza tukafika huko, na dalili zipo, lakini pia tunaweza tukafika huko
kitakwimu tu wakati ukweli na uhalisia wa mambo ni tofauti. Utofauti
ninaouzungumzia ni pale takwimu zitakapoonyesha kwamba sisi ni nchi ya kipato
cha kati wakati mapato halisi na hali za maisha ya watu wengi hazifanani na
takwimu hizo.
Tamaa yangu na kwa kweli jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano, zitakuwa katika
ujenzi wa uchumi wa kipato cha kati ambapo sura na maisha ya Watanzania walio
wengi yafanane fanane na nchi ya kipato cha kati. Njia moja ya kutufikisha huko
ni uendelezaji wa viwanda.
Mheshimiwa Spika;
Tutahakikisha suala la viwanda linasimamiwa vizuri na tunafanikiwa. Matarajio
yangu ni kuwa Bunge lako Tukufu litatuunga mkono mimi na Serikali nitakayoiunda
katika kufikia lengo hili.
Mheshimiwa Spika;
Kama nilivyosema wakati wa Kampeni, na nataka nirudie hapa, tutaanza na viwanda
vilivyopo na kuhakikisha vinafanya kazi. Wale wote ambao walibinafsishiwa
viwanda vilivyokuwa vya umma kwa makubaliano kwamba wataviendeleza niliwataka
wafanye hivyo mapema. Na hapa nataka nisisitize wito wangu huo kwao. Najua huko
nyuma ufuatiliaji na usimamizi wa utekelezaji wa mikataba ya aina hiyo umekuwa
ukilegalega na watu wamejifanyia mambo watakavyo.
Wapo walioacha kabisa uzalishaji na kufumua hata mitambo ya uzalishaji. Mimi
niliahidi, na nataka niseme hapa kwa wazi kabisa, kwamba wale waliobinafsishiwa
viwanda hivyo waanze kazi, waanze kazi mara moja. Wakishindwa basi tutavitwaa
viwanda hivyo kwa kuzingatia sheria na taratibu za nchi na kuwapa watu wengine
wenye nia ya kuviendeleza.
Hatuwezi kuwa na watu wanajiita wawekezaji tunawapa viwanda vyetu halafu
wanaviatamia tu. Mimi hilo sitalikubali na wala sitalivumilia. Nimeielekeza
Ofisi ya Msajili wa Hazina kuanza kushughulikia suala hili mara moja. Naomba
Bunge lako lituunge mkono.
Mheshimiwa Spika;
Njia ya pili ya kuendeleza viwanda ni kuhimiza na kushawishi wawekezaji
kuwekeza katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu. Kama nilivyoeleza miundombinu
ya kufanya hivyo tayari ipo na baada ya muda itakuwa bora zaidi. Najua wapo
watu wanaotaka kuwekeza Tanzania sasa, katika viwanda, na wamekuwepo hata miaka
ya nyuma kidogo, lakini wakati mwingine sisi humu humu ? tukiwemo sisi viongozi
kwa kushirikiana na wafanyabiashara matapeli na laghai ? tumehujumu mipango na
shauku ya wawekezaji wa nanma hiyo.
Pamoja na shauku na utayari wao wa kuwekeza Tanzania tumewawekea vikwazo na
kuwapiga vita na hivyo kuwalazimisha kwenda kuwekeza katika nchi jirani. Sisi
katika Serikali ya Awamu ya Tano tutajitahidi sana kuondoa usumbufu na urasimu
wa aina hiyo na kuongeza bidii ya kuwashawishi wawekezaji wa ndani na wa nje
kuja kuwekeza viwanda hapa nchini. Kwa watendaji wa Serikali watakaokwamisha
jitihada za uwekezaji na ujenzi wa viwanda hapa nchini hatutawavumilia.
Mheshimiwa Spika;
Ni viwanda vya aina ipi hasa tunavyovikusudia? Sura ya kwanza ya viwanda
tunavyovikusudia ni vile ambavyo sehemu kubwa ya malighafi yake itatoka ndani,
hususan kweye sekta za kilimo, mifugo, uvuvi, na madini ? na maliasili
nyingine. Viwanda vya aina hii vitatupa fursa ya kujenga mfumo wa uzalishaji
ndani ya nchi uliofungamana na kushikamana.
Viwanda vya aina hii vitahitaji na kutegemea malighafi toka kwa wazalishaji wa
sekta nilizozitaja, na kwa kufanya hivyo wazalishaji hao watakuwa na soko la
uhakika humu humu ndani ya nchi. Sura ya pili ya viwanda hivi ni kuzalisha
bidhaa ambazo zinatumiwa na watu wengi humu nchini (mass consumption) ? yaani
bidhaa kama vile nguo, viatu, mafuta ya kupikia, n.k. kwa hivyo viwanda hivi
vitakuwa na uhakika wa soko la ndani kabla ya kufikiria soko la nje. Viwanda
hivi vitatarajiwa kuzalisha ziada kwa ajili ya masoko ya nje.
Yote mawili yakitokea, yaani kuzalisha kwa ajili ya soko la ndani na nje,
itatuongezea akiba yetu ya fedha za kigeni na kutuwezesha kutekeleza na
kuendeleza mipango mingine kwa ajili ya ustawi wa uchumi wetu. Sura ya tatu ya
viwanda tunavyovikusudia ni kuzalisha ajira nyingi. Shabaha yetu ni kuwa
ifikapo mwaka 2020 idadi ya ajira itokanayo na viwanda ifikie asilimia 40
ya ajira zote zitakazokuwepo nchini wakati huo.
Mheshimiwa Spika;
Nimeamua kulisema hili kwa kirefu sana kwa sababu ili tufanikiwe lazima
tuelewane na tusaidiane kulisukuma kwa pamoja jambo hili.
Kilimo, Mifugo na Uvuvi
Mheshimiwa Spika;
Sekta nyingine ambazo lazima tutazitilia mkazo mkubwa na kuziendeleza ni
kilimo, mifugo na uvuvi. Tutaziangalia sekta hizi kwa mtazamo wa kibiashara na
viwanda kwa lengo la kuwa na viwanda vya kisasa vya kuongeza thamani mazao
yatokanayo na kilimo, mifugo na uvuvi. Nchi yetu kwa kiasi kikubwa ni nchi ya
kilimo, ufugaji na uvuvi.
Hii inatokana na ukweli kwamba sehemu kubwa ya watu wetu wapatao asilimia 75
wanaishi vijijini na wanategemea kilimo, ufugaji na uvuvi kwa ajili ya maisha
yao. Wakulima, wafugaji na wavuvi wanatumia zana na mbinu duni katika shughuli
zao na wanazalisha zaidi ya asilimia 95 ya chakula chote kinacholiwa
hapa nchini, na kutoa mchango wa asilimia 25 kwenye pato la taifa yaani
GDP, na asilimia 30 ya mapato yetu ya fedha za kigeni.
Kwa takwimu hizi chache ni wazi kwamba mchango wa sekta ya kilimo, mifugo na
uvuvi katika uchumi wetu na maisha yetu ni mkubwa sana. Nichukue nafasi hii
kuwapongeza na kuwashukuru wakulima, wafugaji na wavuvi wote wa Tanzania kwa
mchango wao mkubwa katika maisha yetu na uchumi wa nchi yetu. Nataka kuahidi
kwao sitawaangusha.
Mheshimiwa Spika;
Pamoja na umuhimu wa kilimo, mifugo na uvuvi katika uchumi wetu wakulima,
wafugaji na wavuvi wetu wengi bado ni watu maskini. Mapato yao yako chini na
wanaishi maisha duni. Lengo letu ni kuuimarisha sekta hizi ili ziweze kutoa
mchango mkubwa zaidi katika uchumi wa nchi lakini pia ziweze kuwanufaisha
wakulima, wafugaji na wavuvi katika kuyabadili maisha yao.
Tukiweza kuboresha sekta hizi vijana wengi zaidi watavutiwa kujiunga nazo na
hivyo kupunguza tatizo la upatikanaji wa ajira. Nataka niwahakikishie wakulima,
wafugaji na wavuvi wetu kwamba ahadi zetu kwao tutahakikisha zinatekelezwa.
Serikali ya Awamu ya Tano itazisimamia kwa dhati ahadi hizo ili kuhakikisha
kwamba kilimo, ufugaji na uvuvi unakuwa wa kisasa zaidi na wenye tija.
Baadhi ya mambo tuliyowaahidi kuyatekeleza ni pamoja na haya yafuatayo:
1. Kuwapatia mafunzo ya kilimo, ufugaji na uvuvi wa kisasa ikiwa pamoja na
ufugaji wa samaki,
2. Kuwapatia pembejeo,
3. Kuwapatia zana za kisasa za kilimo, ufugaji na uvuvi,
4. Kuwapatia wataalamu wa ugani,
5. Kuwawezesha kupata masoko ya uhakika ya mazao yao,
6. Kuwapatia mikopo, na kwa hili Benki ya Kilimo itasaidia sana kufikia lengo
hili,
7. Kuondoa ushuru, kodi na kero mbalimbali za mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi
zinazosababisha bei ya mazao hayo kuwa chini (mfano. Kahawa, kule Kagera ina
kodi 26 ambazo husababisha wananchi kuuza kahawa yao Uganda ambako bei iko juu,
tutapunguza kama sio kuondoa kabisa ushuru hizo ili wakulima wapate bei nzuri.
Tutafanya hivyo pia kwa mazao mengine kama mahindi, chai, pamba, korosho,
mkonge, ngozi, nyama, maziwa, samaki, n.k.),
8. Kuwahakikishia umiliki wa ardhi na kuwaondolea usumbufu wa wao kuondolewa
kwenye ardhi zao kupisha wawekezaji,
9. Kuhakikisha kwamba migogoro ya ardhi baina ya wakulima na wafugaji
tunaitatua na kuikomesha kwa kuhakikisha kuwa vyanzo vya msingi vya migogoro
hiyo tunaviondosha haraka,
10. Kuhakikisha kwamba tatizo la wavuvi kuvamiwa na majambazi na uvuvi
haramu linashughulikiwa kikamilifu.
Tatizo la Umaskini na Ajira
Mheshimiwa Spika;
Nimezungumzia umuhimu wa kuendeleza viwanda, kilimo, mifugo na uvuvi kwa sababu
ya matatizo makubwa mawili yanayoikabili nchi yetu kwa sasa. Kwanza, ni tatizo
la UMASIKINI na pili ni tatizo la AJIRA. Ni kweli uchumi wetu
umekuwa ukikua kwa kasi ya kuridhisha, lakini kasi hiyo haijawiana na kasi ya
kuondoa umasikini na uzalishaji wa ajira za kutosha kwa vijana wetu wanaoingia
kwenye soko la ajira kila mwaka.
Mheshimiwa Spika;
Kwa mujibu wa takwimu zilizopo zaidi ya asilimia 28.2 ya Watanzania ni
maskini. Na kwamba kwa namna na kadri uchumi wetu unavyokuwa pengo baina ya
matajiri (walionacho) na maskini (wasionacho) linazidi kukua. Tukiendelea hivi
tunavyoendelea sasa hatutakuwa tunaitakia mema nchi yetu kwa sababu mgawanyiko
mkubwa wa kimapato na tofauti kubwa za kimaisha baina ya matajiri na maskini
ukiachiwa uendelee na kuzidi kukua utachochea chuki na uhasama baina ya
walionacho na wasionacho.
Lazima tujizatiti na kutumia akili, maarifa na nguvu zetu zote kukabiliana na
kuibadilisha hali hii. Kwanza, lazima tushughulike na UMASIKINI wa watu
wetu. Na njia moja kama nilivyokwisha eleza ni uendelezaji wa sekta ya viwanda
na uboreshaji wa sekta za kilimo, mifugo na uvuvi.
Mheshimiwa Spika;
Tatizo la pili ni AJIRA. Kama nilivyokwisha kugusia, ukuaji wa uchumi
wetu haujaenda sambamba na kasi ya watu wanaoingia kwenye soko la ajira kila
mwaka. Tatizo la ajira ni kwa vijana wote waliosoma viwango mbalimbali vya
elimu na wasio na ujuzi. Hii inamaana kwamba sekta zinazochangia kukua kwa
uchumi wa nchi yetu sizo zinazozalisha ajira kwa wingi. Ndio maana ya kuweka
msisitizo kwenye sekta ya viwanda hasa vile vinavyoajiri watu wengi, na sekta
ya kilimo, uvuvi na mifugo ambavyo ndio mwajiri mkubwa hivi sasa.
Mheshimiwa Spika;
Pamoja na kuweka msisitizo katika Viwanda, Kilimo, Mifugo na Uvuvi hatuna budi
kuwawezesha vijana wetu kuanzisha shughuli mbalimbali za uzalishaji kwa viwango
mbalimbali. Ili hili liwezekane, na sisi tutalifanya, linahitaji mambo mawili
makubwa.
Kwanza, kuwaandaa vijana wetu vizuri kielimu na kiujuzi. Hatuna budi
kuweka mkazo katika viwango vya ubora vya elimu na stadi za kazi wanazopata
vijana wetu. Nalisema hili kwa sababu hatuwezi kuzungumzia uendelezaji wa
viwanda ikiwa hatujaandaa vijana wenye uwezo, ujuzi, na stadi za kufanya kazi
hizo kwa ubora na ufanisi wa hali ya juu; hatuwezi kutaka kuwekeza katika
viwanda vya nguo au samani ikiwa hatuna wahandisi wa mitambo wazuri, wabunifu
wa zuri na wenye viwango vinavyotakiwa na kukubalika.
Aidha hatuwezi kuwa na vijana wenye uthubutu wa kuanzisha shughuli za
uzalishaji kama hawana elimu na maarifa ya kubuni miradi na kuiendeleza. Kwa
hivyo tutaelekeza nguvu zetu katika kuhakikisha kuwa shule na vyuo vyetu katika
ngazi mbalimbali vinafundisha na kutoa vijana wenye viwango vya hali ya juu vya
elimu, maarifa, ujuzi na ufundi.
Mheshimiwa Spika;
Pili, ni suala la uwezeshaji wa vijana hasa wale watakaotaka kujiajiri.
Katika kutekeleza lengo hili Serikali ya Awamu ya Tano itachukua na kutekeleza
hatua mbalimbali ikiwemo:
- Kuwawezesha vijana wanaohitimu Elimu ya Juu na Vyuo vya
Ufundi kupata mitaji ya kuwasaidia kuanzisha makampuni yao kulingana na
fani walizosomea;
- Kuwawezesha vijana kuanzisha SACCOS zao na kupitia SACCOS
hizo kuwawezesha kupata mikopo;
- Kuwawezesha vijana wajasiriamali kujiunga na Mifuko ya
Hifadhi ya Jamii ili waweze kupata mikopo na kunufaika na mafao mengine
katika mifuko hiyo.
Mheshimiwa Spika;
Tatu, ni kuzitambua na kuziheshimu kazi na shughuli mbalimbali
zinazofanywa na makundi mbalimbali ya kinamama na vijana. Hapa namaanisha
shughuli za kina Mama lishe, wachuuzi mbalimbali, Machinga, waendesha Boda Boda
na Maguta, na vijana wa kike na wa kiume wanaojitafutia kazi mbalimbali halali
za kujipatia mapato kwa ajili ya kuendesha maisha yao, n.k. Shughuli za makundi
haya zinatusaidia sana katika kupunguza makundi ya vijana wetu ambao wangekaa
tu na kuzurura zurura ovyo bila shughuli ya kufanya. Na kwa kuwa kwa sasa uwezo
wetu wa kuwapatia ajira tofauti ni mdogo ni jukumu letu kuwasaidia na
kuwawezesha kufanya shughuli zao kwa utilivu bila bugudha.
Niliahidi, na nataka nirudie hapa, kwamba Serikali ya Awamu ya Tano
ikishirikiana na Halmashauri zetu, pamoja na Wakuu wa Mikoa na Wilaya itaweka
mipango na taratibu nzuri na rafiki kwa aina ya shughuli ambazo baadhi
nimezigusia. Aidha, ushuru usio wa lazima na wenye usumbufu kwa wafanyabiashara
wadogo wadogo utokanao na shughuli nilizozitaja tutauondoa.
Tunaamini ikiwa tutaweza kuongeza ukusanyaji mapato, na kuziba mianya ya
wakwepaji wakubwa wa kodi ambao huipotezea Serikali mabilioni ya fedha tutakuwa
hatuna sababu ya kufukuzana na kina mama na vijana mitaani. Viongozi na
watendaji wa Serikali na hasa wa Halmashauri watenge maeneo kwa ajili ya
wafanyabishara wadogo na waandae mipango ya kupunguza ushuru usio wa lazima.
Afya
Mheshimiwa Spika;
Dhamira ya kujenga uchumi wa kisasa na suala la kupambana na umasikini
linakwenda sambamba na kuwa na wananchi wenye afya bora. Kwa kutambua ukweli
huu na mahitaji ya huduma bora za wananchi wetu Serikali ya Awamu ya Tano
itahakikisha kwamba wananchi wanapata huduma bora za afya kwa kufanya baadhi ya
mambo yafuatayo:
- Kwanza,
kuimarisha huduma za afya pale zilipo na kuanzisha pale ambapo hazipo.
Lengo ni kuhakisha kwamba kila kijiji kinakuwa na Zahanati, kila Kata
inakuwa na Kituo cha Afya, kila wilaya inakuwa na Hospitali, na kila Mkoa
unakuwa na hospitali ya Rufaa.
- Pili,
tutaimarisha na kuboresha huduma za afya kwa kuongeza utaalamu katika
Nyanja za afya kwa kuwapatia mafunzo watumishi wake ndani na nje ya nchi;
kwa kuzipatia vifaa bora na vya kisasa hospitali, vituo vya afya na
zahanati zetu. Lengo la kufanya hivyo ni kuwezesha upatikanaji wa huduma
mahsusi hapa hapa nchini na hivyo kutolazimika kupeleka watu wetu kutibiwa
nchi za nje.
- Tatu, tutaongeza
bajeti ya dawa na kuboresha mfumo wa upatikanaji ili kuhakikisha dawa
zinapatikana katika hospitali, vituo vya afya na zahanati zetu. Aidha,
tutahamasisha wananchi wajiunge na Bima ya Afya.
Elimu
Mheshimiwa Spika;
Natambua juhudi kubwa zimefanyika katika upanuzi wa elimu ya awali, msingi,
sekondari na vyuo vikuu. Serikali ya Awamu ya Tano itajielekeza katika kuongeza
ubora wa elimu inayotolewa ikiwa pamoja na na kuongeza mkazo katika masomo ya
sayansi. Aidha, tutahakikisha kwamba vifaa vya kufundishia na kujifunzia
vinapatikana ikiwa ni pamoja na maabara, vitabu, madawati, n.k. Tutahakikisha
kuanzia Januari mwakani elimu kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne
inatolewa bure, kama tulivyoahidi kwenye kampeni.
Tutahakikisha kwamba wanafunzi wengi zaidi wa elimu ya juu wanapata mikopo kwa
wakati. Tutashughulikia maslahi na kero za walimu wa ngazi zote ikiwa ni pamoja
na kujenga nyumba za walimu vijijini na kuiunga mkono Benki ya walimu ili iweze
kuwanufaisha zaidi.
Maji
Mheshimiwa Spika;
Wakati wa kampeni nimekutana na malalamiko mengi sana ya ukosefu wa maji.
Serikali ya Awamu ya Tano itahakikisha kwamba inaongeza kiwango cha upatikanaji
wa maji kufikia asilimia 85 kwa maeneo ya vijijini na asilimia 95
kwa maeneo ya mijini ifikapo 2020. Tutakamilisha miradi iliyokwishaanza na
kuanzisha miradi mipya mikubwa na midogo ya maji kutoka katika mito, maziwa na
vyanzo vingine vya uhakika vya maji ikiwa pamoja na kuvuna maji ya mvua.
Tunataka tuwatue akina mama ndoo kichwani. Tunatambua umaskini hauwezi kuondoka
nchini kama wananchi hawapati maji safi na salama.
Umeme
Mheshimiwa Spika;
Suala la upatikanaji wa umeme limeendelea kuwa tatizo katika nchi yetu pamoja
na jitihada kubwa zilizofanywa na Serikali zilizopita. Hatuwezi kuzungumzia
suala la kujenga viwanda wakati umeme hautoshi. Serikali yangu itahakikisha
kwamba umeme unapatikana wa kutosha na wa uhakika. Tutakamilisha miradi ya
umeme iliyopo na kujenga mingine mingi mipya ili wananchi wengi zaidi wanufaike
na nishati ya umeme na viwanda vingi zaidi vidogo vidogo, vya kati na vikubwa
vianzishwe.
Madawa ya Kulevya
Mheshimiwa Spika;
Madawa ya kulevya yamekuwa ni janga kubwa kwa taifa letu na kundi
linaloathirika zaidi ni vijana wa kiume na kike. Familia nyingi zimeathirika na
nguvu kazi ya taifa imepotea. Tutaushughulikia mtandao huo hususan
wafanyabiashara wakubwa wanaojihusisha na madawa ya kulevya bila ajizi.
Mheshimiwa Spika;
Masuala mengine tutakayoyawekea mkazo katika utawala wa Awamu ya Tano ambayo
ninaamini yatasaidia katika kujenga uchumi wetu ni pamoja na masuala ya Utalii,
Mawasiliano, Madini, Ardhi na Makazi, Ujenzi na Miundombinu, Bandari, Barabara,
Ulinzi na Usalama, utunzaji wa mazingira, Vijana, Wanawake, Watu wenye Ulemavu
na Ualbino, Wazee, Wafanyakazi, Wasanii na Wanamichezo, wanahabari,
wafanyabiashara, wawekezaji, wajasiriamali, sekta binafsi, n.k. Utekelezaji wa
masuala haya umefafanuliwa vizuri katika Ilani ya CCM ya mwaka 2015.
Tutayatekeleza ipasavyo.
Mapambano Dhidi ya Rushwa na Ufisadi
Mheshimiwa Spika;
Jambo moja nililolisemea kwa nguvu kubwa wakati wa kampeni ni mapambano dhidi
ya rushwa na ufisadi. Sikufanya hivyo kwa sababu nilitaka tu kuwarubuni
wananchi ili wanipe kura zao na kunifanya kuwa Rais wao. Nililiongea jambo hili
kwa dhati kabisa, na nilichokisema na kuwaahidi wananchi ndicho hasa
nilichokikusudia.
Mheshimiwa Spika;
Wananchi wanachukia sana rushwa na ufisadi, na wamechoshwa na vitendo hivyo.
Mimi pia ninachukia rushwa na ufisadi. Sifurahishwi kabisa na vitendo vya
rushwa na ufisadi vinavyoendelea hapa nchini. Vitendo vya rushwa na ufisadi
vinawanyima haki wananchi na kuitia hasara serikali kwa mamilioni ya fedha
ambazo zingeweza kutumika kwa ajili ya kujenga miradi ya maendeleo kwa ajili ya
watu wetu.
Mheshimiwa Spika;
Chama changu, Chama cha Mapinduzi, kimejengwa katika misingi ya kukataa rushwa
na ufisadi. Ndio maana moja ya Imani kuu za CCM ni ile isemayo: ?Rushwa
ni adui wa haki, sitatoa wala kupokea rushwa?
Kwa Mtanzania mwaminifu kwa imani yake hatakuwa na kigugumizi katika kuwa
mstari wa mbele katika kupambana na rushwa na ufisadi.
Mheshimiwa Spika;
Mmoja wa waasisi wa Taifa letu, Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage
Nyerere, aliwahi kuifananisha rushwa na ufisadi ?Kama Adui Mkubwa wa Watu?.
Akiongea Bungeni Mei 1960, Mwalimu Nyerere alisema yafuatayo kuhusu rushwa:
?Rushwa [na ufisadi] havina budi kushughulikiwa bila huruma kwa sababu
naamini wakati wa Amani rushwa na ufisadi ni adui mkubwa kwa ustawi wa watu
kuliko vita.?
Mheshimiwa Spika;
Haya ni maneno makali ya mtu na kiongozi aliyeichukia na kuikemea rushwa katika
maisha yake yote ya uongozi. Ni maneno yanayotukumbusha tu nini kinaweza
kikatutokea kama taifa endapo tutaendekeza rushwa na ufisadi. Chuki za wananchi
dhidi ya rushwa na ufisadi ni dhahiri, wamechoka kabisa, wamechoka sana, hawako
tayari kuvumilia upuuzi wa serikali itayoonea haya rushwa na kulea mafisadi.
Mheshimiwa Spika;
Mimi nimewaahidi wananchi, na nataka niirejee ahadi yangu kwao mbele ya Bunge
lako tukufu, kwamba nitapambana na rushwa na ufisadi bila kigugumizi na bila
haya yoyote. Dawa ya jipu ni kulitumbua, na mimi nimejipa kazi ya kuwa mtumbua
jipu. Najua kutumbua jipu kuna maumivu lakini bahati mbaya halina dawa
nyingine. Hivyo ninaomba Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wote mniombee na
muniunge mkono wakati natumbua majipu haya.
Mheshimiwa Spika;
Ninafahamu ugumu wa vita niliyoamua kuipigana. Nasema nafahamu ugumu na
changamoto zake kwa sababu wanaojihusisha na rushwa sio watu wadogo wadogo.
Vitendo vya rushwa na ufisadi vyenye madhara makubwa kwa nchi na ustawi wa nchi
yetu hutendwa na watu wenye dhamana kubwa za uongozi na utumishi ambazo
wamezipata kutokana na ridhaa ya watu. Kwa hivyo ili niweze kufanikiwa lazima
nipate ushirikiano mkubwa toka kwa Bunge lako tukufu na vyombo vingine
vilivyopo na vyenye majukumu ya kupambana na vitendo hivi.
Aidha, tutashinda vita hii endapo wananchi pia watatuunga mkono. Sina mashaka
kuwa kwa vile wao, kwa wingi wao, wanachukia rushwa na ufisadi, watakuwa tayari
kutoa ushirikiano wao katika mapambano haya dhidi ya rushwa na ufisadi.
Mheshimiwa Spika;
Katika kushugulikia tatizo hili nimeahidi kuunda mahakama ya Rushwa na Ufisadi.
Ni matumaini yangu vyombo husika katika jambo hili havitanikwamisha.
Aidha, nataka niahidi mbele ya Bunge lako tukufu kwamba, kiongozi yeyote wa
kuteuliwa, ambaye mimi nitakuwa nimemteua kwa mamlaka niliyonayo kikatiba, na
ninayo mamlaka ya kumwajibisha, pindi tu nikibaini na kujiridhisha kuwa
anajihusisha na vitendo vya rushwa na ufisadi nitamtimua mara moja. Baada ya
mimi kuchukua hatua hizo hatua na taratibu zingine za kisheria zitafuata.
Mheshimiwa Spika;
Ninachotaka kusema ni kuwa Serikali yangu itafuatilia kwa karibu mienendo ya
viongozi na watendaji wake ili kubaini kwa haraka nani anajihusisha na vitendo
vya rushwa na ufisadi. Na tukishajiridhisha hatutasubiri, tutachukua hatua. Ni
imani yangu wengine pia katika ngazi mbalimbali mtafanya hivyo. Kwa sababu bila
kufanya hivyo rushwa na ufisadi vitazoeleka na kuwa wimbo unaoburudisha badala
ya kuudhi na kukera.
Muundo wa Serikali na Utumishi
Mheshimiwa Spika;
Nilipokuwa nazunguka na kuzungumza na wananchi wakati wa Kampeni za Uchaguzi,
niliahidi kuwa nitaunda serikali ndogo ya wachapa kazi.
Aidha, niliahidi pia kuunda serikali ambayo itawatumikia watu na hasa wananchi
wa kawaida. Serikali nitakayounda, nataka iwe inawahudumia wananchi kwa haraka
na sio kuwasumbua sumbua na kuwazungusha. Natoa rai kwa watumishi wa serikali,
hasa ambao ni wazembe na wavivu, kujiandaa. Wamevumiliwa kwa muda mrefu sasa
basi. Kwa sababu watumishi wa aina hiyo hawatavumuliwa katika serikali
nitakayoiongoza.
Lugha za ?hiyo ni changamoto tutaishughulikia?, au ?Mchakato
unaendeela? hazitavumiliwa katika Serikali ya Awamu ya Tano. Mimi
nataka watu wa Kazi Tu. Hatuwezi kulea watu ambao wanalipwa mishahara
lakini hawafanyi kazi wanazotakiwa kufanya, au wamegeuza ofisi za umma kuwa ni
mahala pa kuchuma bila kufanya kazi.
Mheshimiwa Spika;
Pamoja na kuwataka watumishi wa Serikali kufanya kazi hatuna budi kuyaangalia
na kuboresha mishahara na maslahi yao na mazingira yao ya kufanyia kazi kwa
kuwapatia vitendea kazi bora na vya kisasa. Na jambo moja
tutakalolitekeleza ni kuangalia namna ya kupunguza kodi ya mapato katika
mishahara ya wafanyakazi yaani PAYE. Pia tutajitahidi kuwatambua na
kuwapa motisha wafanya kazi wachapa kazi.
Kuongeza Mapato na Kupunguza Matumizi ya Serikali
Mheshimiwa Spika;
Kwa zaidi ya miaka mitatu sasa ukusanyaji wa mapato umekuwa chini ya makadirio
kwa sababu mbalimbali. Serikali ya Awamu ya Tano itaongeza nguvu katika upanuzi
wa wigo wa kodi na kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato. Tutahakikisha
kwamba kila mtu anayestahili kulipa kodi analipa kodi stahiki. Hatutasita
kumchukulia hatua mtu yoyote atakaye kwepa kulipa kodi. Tunawaomba wananchi
mhakikishe mnapewa risiti kila mnaponunua bidhaa au huduma.
Kodi ni kitu muhimu lazima kila mtu anayestahili kulipa kodi alipe.
Aidha, tutahakikisha kwamba kila senti inayoongezeka katika mapato ya Serikali
inaelekezwa katika kutoa huduma bora zaidi kwa wananchi. Tutaziba mianya ya
upotevu wa fedha za Serikali ambayo inaipunguzia Serikali uwezo wake wa
kuwahudumia wananchi.
Mheshimiwa Spika;
Nitataja baadhi tu ya maeneo ambayo tutayasimamia kwa lengo la kupunguza
matumizi yasiyo ya lazima na kuziba mianya ya uvujaji wa fedha za Serikali:
Kwanza, safari zote zisizo za lazima nje ya nchi Serikalini
tutazidhibiti na badala yake tutawatumia mabalozi wetu kutuwakilisha kwenye
mikutano ya aina hiyo. Na pale inapolazimu kiongozi au mtumishi mwandamizi
kusafiri tutahakikisa kwamba haandamani na msururu wa watu wengi ambao hawana
umuhimu wala shughuli za kufanya katika safari hizo.
Katika kusisitiza hili napenda niwape takwimu za fedha zilizotumika ndani ya
Serikali, Mashirika ya Umma na Taasisi nyingine za Serikali kwa safari za nje
kati ya mwaka 2013/14 na 2014//2015. Jumla ya shilingi bilioni
356.324 zilitumika kwa ajili ya safari za nje kama ifuatavyo:
- Tiketi za ndege (Air ticket) zilitumia shilingi
bilioni 183.160;
- Mafunzo nje ya nchi (Training Foreign) zilitumia
shilingi bilioni 68.612;
- Posho za kujikimu (Per Diem Foreign) zilitumia
shilingi bilioni 104.552;
Wizara na Taasisi zinazoongoza kwa matumizi ya safari za nje ni pamoja na
Bunge, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikano wa Kimataifa, Wizara ya Fedha,
Ofisi ya Waziri Mkuu, Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali (NAOT),
Wizara ya Mambo ya Ndani, n.k.
Hizi fedha zingeweza kutumika vizuri kuboresha huduma za wananchi wa maisha ya
chini, kama afya, maji, elimu, umeme n.k. Mfano; fedha hizi zingetosha
kutengeneza kilometa 400 za barabara za lami, tujiulize zingeweza
kutengeneza zahanati ngapi?, nyumba za walimu ngapi?, madawati mangapi? n.k.
Hivyo tunapodhibiti safari za nje tunawaomba Waheshimiwa Wabunge na Watanzania
wote mtuelewe na mtuunge mkono.
Pili, tutahakikisha tunadhibiti safari na ziara za mafunzo nje ya nchi
zinazogharamiwa na serikali ambayo yanapatikana hapa nchini.
Tatu, tutadhibiti warsha, semina, makongamano, na matamasha ambayo kwa
kweli yanatumia fedha nyingi tu za serikali lakini hayana tija na wala
hayaongezi ufanisi katika utekelezaji na usimamizi wa sera na mipango ya
Serikali.
Nne, tutasimamia kwa ukamilifu Sheria ya Manunuzi ya Umma ili
kuhakikisha kwamba mianya yote ya fedha za umma inayotokana na usimamizi hafifu
tunaiziba. Ni matarajio yangu kutakapoleta Mswada wa Marekebisho ya Sheria ya
Manunuzi ya Umma Waheshimiwa Wabunge mtatuunga mkono.
Tano, tutasimamia na kudhibiti ukiukwaji wa maagizo na maelekezo
mbalimbali yaliyokwisha kutolewa na Serikali siku za nyuma kuhusu ununuzi wa
bidhaa kama samani kwa ajili ya matumizi ya Serikali. Samani zote kwa ajili ya
matumizi ya Serikali zinatakiwa ziwe zile zinazozalishwa hapa hapa nchini.
Sita, Serikali ya Awamu ya Tano itasimamia kwa karibu na kuthibiti
ununuzi wa magari ya gharama kwa ajili ya Viongozi na Watumishi waandamizi wa
Serikali; na
Saba, tutaendelea kuchunguza na kudhibiti matumizi ya Serikali na
Taasisi zake zote yasiyo na tija kwa uchumi wa taifa letu.
Mheshimiwa Spika;
Kwa ajili hiyo, vipaumbele vya Serikali ninayotarajia kuiunda vitakuwa ni: kupunguza
urasimu ili kuongeza kasi ya utekelezaji wa maamuzi na miradi ya Serikali; kubana
matumizi kwa kupunguza yale ambayo kutokana na hali yetu ya uchumi kwa sasa
yanaweza kuepukika; na kurejesha nidhamu ya Serikali na utumishi wa umma
kwa kuongeza uwazi na uwajibikaji.
Tutatekeleza vipaumbele hivyo kwa kufanya pamoja na mambo mengine kupunguza
ukubwa wa Baraza la Mawaziri; kuongeza usimamizi katika ukusanyaji wa mapato ya
kodi na maduhuli ya Serikali kwa kuziba mianya ya ukwepaji kodi, tutahakikisha
kwamba wale wote wanaotakiwa kulipa kodi wanalipa ipasavyo. Tutaongeza nidhamu
ya matumizi ya Serikali ili kuhakikisha fedha zinazookolewa zinakwenda kwenye
miradi ya maendeleo; na kusimamia sheria, kanuni na taratibu za uwajibikaji wa
viongozi na watumishi wa umma ili wawajibike kwa wananchi ambao ndio wateja na
waajiri wakuu wa watumishi wa umma. Serikali ya Awamu ya Tano itaendelea
kubainisha maeneo mengine ya matumizi yasiyo ya lazima ambayo yanaigharimu
Serikali fedha nyingi na kuyadhibiti.
Aidha, nitoe wito kwa Watanzania wote kila mmoja wetu afanye kazi iwe shambani,
ofisini, kiwandani, sokoni, n.k. Badala ya tabia ya sasa iliyoanza kujengeka
kwa Watanzania kutokupenda kufanya kazi na hivyo kupoteza muda mwingi vijiweni,
muda ambao ungetumika kufanya kazi ndiyo maana kauli mbiu yangu ni HAPA KAZI
TU!
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kikanda na Kimataifa
Mheshimiwa Spika;
Nchi yetu imepata mafanikio makubwa katika Nyanja ya diplomasia na ushirikiano
wa kimataifa katika awamu zilizotangulia za uongozi. Serikali yangu itaendeleza
sifa hiyo kwa kujenga juu ya msingi imara uliowekwa na awamu zilizotangulia na
awamu ya nne chini ya Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete. Tutaendelea kuwa
waumini na tutaendeleza sera ya ujirani mwema na nchi zinazotuzunguka kwa lengo
la ustawi wa watu wetu na maslahi mapana ya nchi yetu.
Tutaendelea kuwa waaminifu wa utangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC)
na daima tutatekeleza wajibu wetu kwa mujibu wa Mkataba wa Uanzishwaji wa
Jumuiya ya Afrika Mashariki, itifaki zake na maamuzi ya vikao vya nchi
wanachama. Tutaendelea kutekeleza matakwa ya Mkataba huu wa kujenga utengamano
wetu hatua kwa hatua.
Mheshimiwa Spika;
Tanzania itaendelea kuwa mwanachama mwaminifu wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini
mwa Afrika (SADC) na kuendelea kushirikiana kwa karibu na nchi wanachama ambao
tunauhusiano wa kihistoria na kidugu. Tutaendelea kuamini katika Umoja wa
Afrika (AU) na azma ya ndoto ya waasisi wetu ya kuunganisha bara la Afrika.
Tutaendelea pia kushiriki kikamilifu katika Jumuiya ya Nchi za Maziwa Makuu
(ICGLR) na kushirikiana na nchi wenzetu wanachama kutafuta majawabu ya kudumu
ya amani, usalama na maendeleo katika eneo la maziwa makuu.
Tutaendeleza na kustawisha mahusiano na marafiki zetu wote Magharibi, Mashariki
ya Mbali na Mashariki ya Kati kwa lengo la kushirikiana kwa maslahi ya nchi
zetu na watu wetu. Tutapenda kutumia fursa nzuri ya mahusiano yetu mazuri
kisiasa kukuza mahusiano yetu ya uchumi kwa kutumia diplomasia ya uchumi.
Tutafanya hivyo pia kwa ushirikiano wa kimataifa kwa kuendeleza mahusiano yetu
na Umoja wa Mataifa (UN) na taasisi zake, Jumuiya ya Madola, Benki ya Dunia,
Shirika la Fedha Duniani (IMF) na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), n.k.
Aidha, tutazitaka Balozi zetu zionyeshe matunda yanayolingana na thamani ya
fedha tunazowapelekea hususan katika kuvutia uwekezaji, biashara, utalii na
mchango wao katika ukuzaji wa sekta ya viwanda. Tunataka kuona diplomasia yetu
na Sera yetu ya nje ikijibu changamoto zetu za ndani za ajira, miundombinu,
masoko ya mazao ya wakulima, viwanda n.k.
Hitimisho
Mheshimiwa Spika;
Naomba kabla ya kuhitimisha nitoe wito kwa Waheshimiwa Wabunge, Bunge hili
linalo nafasi ya kuweka historia ya kuwa kitu kimoja na kuweka masilahi ya
Taifa mbele. Kama kuna kitu ambacho wananchi wanachukia ni lugha za vijembe,
mipasho, na ushabiki wa vyama bungeni. Kwanza, tukumbuke wote bila kujali
itikadi za vyama vyetu sisi ni kitu kimoja; na pili tumechaguliwa kuwawakilisha
wenzetu. Baada ya miaka mitano kila mmoja atarudi kwenye jimbo lake kuomba kura
na huko atapimwa kwa maendeleo aliyopeleka.
Tusimame pamoja, Tanzania ni yetu sote tutangulize masilahi ya nchi mbele, na
kwa mara ya kwanza Watanzania waone Bunge tofauti na sio Bunge la kuzomea,
kutoka nje, kutukanana, mipasho, n.k. Tunaitwa Waheshimiwa kwa heshima ya
dhamana tuliyopewa na Bunge hili Tukufu, tutunze heshima hiyo ili tuzidi
kuheshimiwa.
Aidha, napenda kusisitiza kuwa kazi iliyoko mbele yetu ni kubwa. Matarajio na
matumaini ya Watanzania waliotuchagua na kutupa ridhaa ya kuwaongoza katika
kipindi cha miaka mitano ijayo ni makubwa. Wanachotaka kuona ni nchi yetu
kupiga hatua kubwa za maendeleo zitakazojibu matumaini yao na kutatua shida na
kero zao. Nyie na mimi, baada ya miaka mitano toka sasa, tutapimwa kwa namna
tutakavyokuwa tumetekeleza mambo ambayo tumewaahidi Watanzania wenzetu.
Mimi nina amini kabisa kwa ushirikiano wetu na kwa kufanya kazi kwa bidii na
ubunifu tutaweza kuzitimiza ndoto za Watanzania wenzetu.
Mheshimiwa Spika;
Sasa natamka kwamba nimelifungua rasmi Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania. Asanteni kwa kunisikiliza!
Mungu libariki Bunge letu na Wabunge wake!
Mungu Ibariki Afrika!
Mungu Ibariki Tanzania!
Ahsanteni kwa kunisikiliza.