 |
Mhe. Rais Dr. Jakaya Mrisho Kikwete akihutubia Bunge la katiba |
HOTUBA YA RAIS WA
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, MHESHIMIWA JAKAYA MRISHO KIKWETE, WAKATI WA
KULIHUTUBIA BUNGE MAALUM LA KATIBA
TAREHE 21MACHI, 2014,
DODOMA
Mheshimiwa Samuel Sitta, Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba;
Mheshimiwa Dkt. Mohamed Gharib Bilal, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania;
Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi;
Mheshimiwa Mizengo Peter Pinda, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa Maalim Seif Sharif Hamad, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar;
Mheshimiwa Balozi Seif Ali Iddi, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
Mheshimiwa Anne Semamba Makinda; Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano;
Mheshimiwa Pandu Ameir Kificho, Spika wa Baraza la Wawakilishi na Mwenyekiti wa
Muda wa Bunge Maalum la Katiba ;
Mheshimiwa Rashid Othman Chande, Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa Othman Makungu, Jaji Mkuu wa Zanzibar;
Viongozi Wakuu Wastaafu;
Waheshimiwa Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba;
Waheshimiwa Wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba;
Wageni waalikwa;
Mabibi na Mabwana;
Pongezi
Nakushukuru sana Mheshimiwa Mwenyekiti kwa kunipa fursa ya kuja kuzungumza na
Waheshimiwa Wajumbe wa Bunge letu Maalum la Katiba katika siku hii muhimu na ya
kihistoria kwa nchi yetu. Nimekuja kuwatakia heri na naungana na Watanzania
wenzetu wote kuwaombea baraka za Mwenyezi Mungu, ili muweze kuifanya kazi yenu
kwa utulivu, hekima, umakini mkubwa na kuimaliza kwa salama na kwa mafanikio
yanayoyatarajiwa na Watanzania.
Natoa pongezi nyingi kwako na kwa Makamu wako kwa kuchaguliwa kwenu kuongoza
Bunge hili maalumu na la kihistoria. Ushindi mkubwa mliopata ni kielelezo tosha
cha imani kubwa na matumaini waliyonayo Wajumbe wenzenu kwenu. Matumaini yao
ndiyo matumaini ya Watanzania wote, kwamba mtaliongoza vizuri Bunge hili, ili
liweze kutimiza kwa ufanisi mkubwa jukumu lake muhimu sana katika historia ya Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Niruhusu pia niwapongeze kwa dhati Wajumbe wote wa Bunge Maalum la Katiba kwa
bahati ya aina yake waliyopata ya kutunga Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania. Fursa hii hutokea mara chache sana katika historia ya nchi yo yote na
watu wake. Mkifanikiwa kuipatia nchi yetu Katiba nzuri majina yenu yataandikwa
kwa wino wa dhahabu, katika kumbukumbu za historia ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania.
Ni matarajio ya Watanzania kuwa mtatunga Katiba itakayokubalika na wengi.
Katiba inayotekelezeka. Katiba itakayoimarisha Muungano wetu kwa kuondoa
changamoto zilizopo sasa. Katiba itakayoipa nchi yetu mfumo bora wa kuongoza na
kuendesha mambo yetu. Katiba itakayoimarisha umoja, upendo, ushirikiano na mshikamano
miongoni mwa wananchi wa Tanzania, licha ya tofauti zao za asili za upande wa
Muungano na maeneo watokako, au tofauti za jinsia, rangi, kabila, dini na
ufuasi wa vyama vya siasa. Katiba itakayodumisha amani, usalama na utulivu
nchini. Katiba itakayostawisha zaidi demokrasia, haki za binadamu, utawala wa
sheria, utawala bora na kudhibiti maovu.
Na, mwisho ingawaje siyo mwisho kwa umuhimu, Katiba itakayoweka mazingira
mazuri kwa uchumi wa nchi kukua, na wananchi wengi kunufaika sawia na maendeleo
yatayopatikana.
Historia ya Katiba Nchini
Mheshimiwa Mwenyekiti na Waheshimiwa Wajumbe;
Hii itakuwa mara ya tatu tangu kuzaliwa kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Aprili 26, 1964, kwa nchi yetu kuwa na mchakato wa kutunga Katiba mpya. Mara ya
kwanza ilikuwa mwaka 1965 ilipotungwa Katiba ya Muda na mara ya pili ni mwaka
1977 ilipotungwa Katiba ya Kudumu tuliyonao sasa. Tofauti na mara mbili
zilizopita, safari hii mchakato unahusisha watu wengi zaidi. Wananchi
wameshiriki moja kwa moja kutoa maoni yao kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, na
ndio watakaofanya uamuzi wa mwisho kuhusu Katiba mpya kwa kura ya maoni.
Wananchi pia walipata nafasi ya kuchagua Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya
Wilaya yaliyojadili Rasimu ya Kwanza ya Katiba. Pia walipata nafasi ya kutoa
maoni yao kupitia Mabaraza ya Katiba ya taasisi. Katika Bunge hili wapo
wananchi 201 kutoka makundi mbalimbali.
Katika mchakato wa kutunga Katiba za mwaka 1965 na 1977 kulikuwapo Tume za
Kuandaa Rasimu na Bunge Maalum la Katiba kama ilivyo katika mchakato huu. Hata
hivyo, kwa Katiba zilizopita Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano pekee ndio
waliounda Bunge Maalum. Safari hii Bunge Maalum linajumuisha Wabunge, Wajumbe
wa Baraza la Wawakilishi na wananchi 201 wanaotoka kwenye jamii, wakiwakilisha
asasi na makundi mbalimbali ya Watanzania kutoka Zanzibar na Tanzania Bara.
Mchakato wa sasa utaishia kwenye kura ya maoni itakayoshirikisha wananchi wote
wa Tanzania wanaoruhusiwa kupiga kura. Michakato iliyopita iliishia Bunge
Maalum pekee.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Tangu kutungwa kwake, tarehe 25 Aprili, 1977, mpaka sasa Katiba ya Jamhuri ya
Muungano ya mwaka 1977 imefanyiwa mabadiliko takriban mara 14. Mabadiliko hayo
yalitokana na kufanyika au kutokea kwa mabadiliko muhimu ya kiuchumi, kisiasa
na kijamii katika nyakati mbalimbali hapa nchini na katika Jumuiya ya Afrika
Mashariki.
Kwa ruksa yako naomba nitaje baadhi ya mabadiliko yaliyofanywa:-
1. Mabadiliko ya 1979 yaliunda Mahakama ya Rufani ya Tanzania kufuatia kufa kwa
Mahakama ya Rufani ya Afrika Mashariki baada ya kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika
Mashariki mwaka 1977.
2. Mabadiliko ya mwaka 1980 yalifanyika baada ya kutungwa kwa
Katiba ya Zanzibar, hivyo kulazimu Katiba hiyo kutambulika kwenye Katiba ya
Jamhuri ya Muungano.
3. Mabadiliko ya mwaka 1984 yaliweka utaratibu wa ukomo wa
vipindi vya Urais ambao haukuwepo kabla ya hapo. Aidha, masuala ya Haki za
Binadamu (Bill of Rights) yaliingizwa kwa mara ya kwanza katika Katiba.
Vilevile, Mahakama ya Rufani ya Tanzania na mambo mengine ya iliyokuwa Jumuiya
ya Afrika Mashariki yaliongezwa katika Orodha ya Mambo ya Muungano.
4. Mwaka 1992, yalifanyika mabadiliko yaliyoanzisha Mfumo wa
Vyama Vingi vya Siasa badala ya ule wa Chama kimoja uliokuwepo tangu 1965. Pia
utaratibu wa uchaguzi wa Rais na Wabunge ulirekebishwa ili uendane na mfumo wa
vyama vingi vya siasa. Vilevile utaratibu wa kuwa na viti maalum vya wanawake
katika Bunge ulianzishwa. Wakati ule ilikuwa asilimia 15 ya Wabunge wote.
Aidha, kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi yetu Bunge lilipewa mamlaka
ya kumwajibisha Rais na Waziri Mkuu kupitia kura ya kutokuwa na imani.
5. Mabadiliko ya mwaka 1994 yaliweka mfumo mpya wa kumpata
Makamu wa Rais kupitia Mgombea Mwenza.
6. Mwaka 2000 na 2005, pamoja na mambo mengine yalifanyika
mabadiliko yaliyopanua wigo wa Haki za Binadamu na kuongeza uwakilishi wa
wanawake.
Umuhimu wa Mabadiliko ya Katiba
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Kufanyika kwa mabadiliko hayo kunathibitisha utayari wa Serikali kufanya
mabadiliko kila ilipoonekana inafaa kufanya hivyo. Pamoja na kufanya yote hayo
na Serikali kuwa na msimamo huo, kumekuwepo na madai yaliyokuwa yanajirudia ya
kutaka Katiba ya Tanzania iandikwe upya. Wako watu walioimithilisha Katiba yetu
na nguo yenye viraka vingi mno kiasi kwamba ingefaa kununua mpya badala ya
kuendelea kuivaa.
Madai ya kutaka Katiba mpya yalipazwa sauti baada ya kuanza kwa mfumo wa vyama
vingi vya siasa. Wapo waliokuwa wanadai Katiba mpya kwa imani, eti kwamba,
itawawezesha kuishinda CCM. Lakini, si hayo tu, hata katika mchakato wa
Serikali zetu mbili kushughulikia kero za Muungano, imedhihirika kuwa baadhi ya
changamoto zilikuwa zinahitaji mabadiliko ya Katiba ili kuzipatia ufumbuzi wa
uhakika na wa kudumu.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Kwa kutambua ukweli huo na baada ya kushauriana na kukubaliana na viongozi
wenzangu wakuu wa Chama tawala na Serikali zetu mbili wakati ule, ndipo tarehe
31 Desemba, 2010, nikatangaza dhamira ya kuanzisha mchakato wa kutunga Katiba
mpya. Nilieleza siku ile kuwa katika mchakato huo tutakuwa na ushirikishwaji
mpana wa wananchi wa Tanzania kwa makundi yao ya jinsia, dini, siasa na
shughuli wazifanyazo kujipatia riziki na kwa maeneo wanayotoka katika pande
zetu mbili za Muungano.
Mchakato wa Katiba Mpya
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Tarehe 16 Machi, 2011 Baraza la Mawaziri liliridhia kutungwa kwa Sheria ya
Mabadiliko ya Katiba ya kuliongoza taifa katika mchakato wa kutunga Katiba mpya
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tarehe 18 Novemba, 2011 Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania lilipitisha Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba. Kwa
mujibu wa Sheria hiyo, mchakato wa kutunga Katiba Mpya ulikuwa unaanza kwa
kuunda Tume ya Mabadiliko ya Katiba. Tume hiyo imepewa jukumu la kusikiliza
maoni ya wananchi mmoja mmoja na kwa makundi yao ya maslahi, taasisi zao na
kupitia Mabaraza ya Katiba. Mwishowe Tume imetakiwa kutengeneza Rasimu ya
Katiba mpya itakayofikishwa kwenye Bunge Maalum la Katiba kujadiliwa na Katiba
mpya kutungwa. Mchakato wa Katiba utahitimishwa kwa wananchi kupiga kura ya
maoni ya kuamua kama wanaikubali au kuikataa Katiba mpya.
Tarehe 6 Aprili, 2012 nilifanya uteuzi wa Wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya
Katiba na kuwaapisha tarehe 13 Aprili, 2012. Tume ilianza kazi tarehe 2 Mei,
2012 na kuikamilisha kwa mafanikio, hatua zote zilizoihusu na kukabidhi kwangu
na kwa Rais wa Zanzibar, Taarifa ya Tume na Rasimu ya Katiba tarehe 30 Desemba,
2013. Kitendo cha Mwenyekiti wa Tume, Mheshimiwa Joseph Warioba kuwasilisha
Rasimu hiyo mbele ya Bunge hili tukufu tarehe 18 Machi, 2014, kinahitimisha
rasmi kazi ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba. Kazi inayofuatia ni ya Bunge hili
kujadili, kuamua na kutunga Katiba mpya. Baada ya hapo Katiba mpya itafikishwa
kwa wananchi kwa uamuzi wa mwisho kwa njia ya kupiga kura ya NDIYO au HAPANA.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Rasimu ya Katiba ilichapishwa kwenye gazeti la Serikali na magazeti mengine
yanayosomwa na wananchi kama ilivyoagizwa katika Kifungu cha 20(2) cha Sheria
ya Mabadiliko ya Katiba. Pamoja na hayo, Taarifa ya Tume na Rasimu ya Katiba
viliwekwa wazi kwenye tovuti ya Tume kwa kila mtu kusoma. Inafurahisha kuona kuwa
watu wengi wameisoma Taarifa ya Tume na Rasimu ya Katiba na kumekuwa na mjadala
mpana kuhusu nyaraka zote hizo muhimu. Watu wengi wametoa maoni yao na
wanaendelea kufanya hivyo. Kwa maoni yangu hili ni jambo jema sana na ni
kielelezo thabiti kuwa demokrasia imestawi na inazidi kuota mizizi Tanzania.
Pia, kwamba, Watanzania wako huru kushiriki na kutoa maoni yao kwa mambo
yanayowahusu.
Pongezi kwa Tume
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Kwa mara nyingine tena narudia kutoa pongezi za dhati kwa Wajumbe wa Tume ya
Mabadiliko ya Katiba chini ya uongozi wa Mheshimiwa Jaji Joseph Warioba
akisaidiwa na Mheshimiwa Jaji Augustino Ramadhani, kwa kazi kubwa na nzuri
waliyofanya. Kazi yao haikuwa rahisi hasa ukizingatia ukubwa wa nchi yetu,
wingi wa watu wake, utitiri wa taasisi na pigo la kumpoteza Mjumbe mwenzao
muhimu Dkt. Sengondo Mvungi aliyetangulia mbele ya haki katikati ya mchakato.
Pamoja na hayo, kwa bidii kubwa Wajumbe wa Tume wameweza kutembelea mikoa yote
nchini na kuwafikia watu 351,644 waliotoa maoni yao kwa mdomo na kwa maandishi.
Halikadhalika, walipokea na kuchambua maoni 772,211 kutoka kwa wananchi na
taasisi mbalimbali. Baada ya kupokea maoni ya wananchi, kufanya utafiti na kwa
kutumia maarifa na uzoefu wao, Wajumbe wakafanya kazi ngumu, kuliko yote, ya
kutengeneza Rasimu ya Katiba iliyoko mbele ya Bunge hili. Ni kweli kwamba
Wajumbe hawakuweza kuwafikia wananchi wote wa Tanzania, lakini wameweza
kuwafikia wananchi wengi, ambao kwa kiasi kikubwa wanawakilisha taswira na
mitazamo mipana ya jamii yetu.
Baadhi ya Masuala Yaliyojitokeza Katika Mjadala wa Mapendekezo ya Tume
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Tume imefanya kazi nzuri, yenye thamani kubwa na ya manufaa kwa taifa la
Tanzania. Rasimu imeandikwa vizuri na kwa weledi wa hali juu. Tume imetoa
mapendekezo ambayo kwa kiasi kikubwa yanahuisha na kuboresha Katiba ya nchi
yetu, kwa namna ya pekee. Katiba inayopendekezwa, imejumuisha dhana na mambo
kadhaa mapya yanayokwenda vyema na wakati tulionao na kuweka msingi mzuri kwa
huko mbele tuendako. Kwa taratibu za kawaida za marekebisho ya Katiba
tuliyonayo, isingekuwa rahisi kuingiza mambo mengi mapya kiasi hiki.
Wajumbe Wana Kazi Kubwa
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Waheshimiwa Wajumbe;
Rasimu ya Katiba ni kitabu kikubwa kilichosheheni mambo mengi. Kina kurasa 106,
sura 17 na ibara 271. Wajumbe wa Bunge hili mnatakiwa kusoma na kuelewa vizuri
kila kilichoandikwa ili muweze kufanya uamuzi ulio sahihi. Mnawajibika
kuchambua kwa kina na umakini mkubwa kila kilichomo, sura kwa sura, ibara kwa
ibara, sentensi kwa sentensi na hata neno kwa neno. Hamna budi kujiridhisha
kuhusu uandishi wa vifungu vya Rasimu ya Katiba na kufaa kwa dhana mbalimbali
zilizoingizwa na kujengeka katika Rasimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Kile ambacho Wajumbe mtaona kinastahili kuboreshwa au kurekebishwa au kufutwa
msisite kufanya hivyo ili Watanzania wapate Katiba iliyo bora. Msipofanya hivyo
kuna hatari ya kupata Katiba ambayo ni ngumu kuitekeleza. Aidha, tunaweza kuwa
na Katiba ambayo itanung’unikiwa na watu wengi na kusababisha madai ya kutaka
ifanyiwe marekebisho muda mfupi baada ya kupitishwa. Bunge hili linao wajibu
maalum wa kuzuia balaa hilo lisitokee katika nchi yetu. Ngazi mbalimbali
zilizowekwa katika mchakato huu ni kama chujio la kuepusha hali hiyo isitokee.
Kile ambacho hakikuonekana katika hatua moja kitaonekana katika hatua
inayofuata na kurekebishwa. Nawaomba fursa mliyonayo muitumie vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Nimekwishaeleza kuwa moja ya jambo mnalotegemewa kufanya ninyi wenzetu mliopewa
dhamana ya kutunga Katiba ya nchi yetu ni kujiridhisha na uandishi wake. Yapo
maoni yaliyotolewa kuhusu uandishi ambayo naomba myatafakari na kuamua
ipasavyo. Kwa mfano, kuna baadhi ya vifungu vya Katiba vinayopendekezwa
vimekuwa na mambo mengi mno kuliko inavyostahili Katiba kuwa (too
prescriptive). Pia kuna mawazo kwamba baadhi ya mambo hayangetakiwa kuwa katika
Katiba bali yawe kwenye Sheria zinazotafsiri utekelezaji wa Katiba yenyewe.
Yako mambo yaliyotajwa kwenye Katiba ambayo yanatakiwa kuelezwa wazi kuwa mtu
hatakwenda mahakamani kuidai Serikali impatie (non justiciable). Mambo
yaliyotajwa kwenye Katiba ni mazuri na yanavutia, lakini lazima yaendane na
uwezo wa nchi na uchumi wake kuhimili. Simaanishi kwamba tuyatoe kwenye Katiba,
bali yabakie kama dhamira pale uwezo wa nchi utakaporuhusu yatekelezwe.
Tusipofanya hivyo, kuna hatari ya Serikali kujikuta inalaumiwa au hata
kufikishwa mahakamani kila wakati kwa madai ya jambo moja au jingine ambayo
haina uwezo nayo. Ni muhimu sana mambo kama hayo muyatazame ili tusije kuwa na
Katiba ambayo ni ngumu kutekeleza.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Yapo pia maoni kuwa baadhi ya vifungu vina upungufu katika uandishi wake, hivyo
kuhitaji kufanyiwa marekebisho. Isipofanyika hivyo kunaweza kuwepo athari na
nyingine zinaweza kuwa mbaya. Kwa mfano, Ibara ya 2 ya Rasimu inayotambulisha
eneo na mipaka ya nchi yetu. Ibara hiyo inasomeka kuwa “Eneo la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania ni eneo lote la Tanganyika likijumuisha sehemu yake ya
bahari na eneo lote la Zanzibar likijumuisha sehemu yake ya bahari”.
Maelezo hayo yameacha kutambua, kwa upande wa Tanzania Bara, sehemu yetu ya
maziwa na mito ambayo ni kubwa sana. Kwa nini tuache kuitaja? Je hatutoi nafasi
kwa nchi tunazopakana nazo siku moja wakaja kupora sehemu zetu hizo na sisi
kukosa utetezi kwa kuwa hata Katiba yetu haikuyatambua maeneo hayo kuwa ni
yetu? Hili ni jambo kubwa ambalo Bunge hili lazima mlirekebishe. Wakati ndiyo
huu hakuna mwingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Jambo jingine kuhusu uandishi ni mgongano kati ya pendekezo la msingi la Tume
la kuwa na muundo wa Serikali tatu na majukumu ya Serikali ya Muungano ambayo
kimsingi ni majukumu ya Serikali za nchi washirika. Katika Rasimu hii malengo
ya taifa yameainishwa na Serikali ya Muungano inatakiwa kuhakikisha kuwa
malengo hayo yanatekelezwa na itoe taarifa Bungeni. Katika mfumo wa Serikali
tatu unaopendekezwa na Tume masuala yahusuyo uchumi na maendeleo ya jamii kama
vile kukuza kilimo, ufugaji, uvuvi, viwanda, biashara, pembejeo, elimu, hifadhi
ya jamii na kadhalika yako chini ya mamlaka ya Serikali za nchi washirika.
Mamlaka ya Serikali ya Muungano ni kwa mambo saba tu yafuatayo:- Katiba na
Mamlaka ya Jamhuri ya Muungano, Ulinzi na Usalama wa Jamhuri ya Muungano, Uraia
na Uhamiaji, Sarafu na Benki Kuu, Mambo ya Nje, Usajili wa Vyama vya Siasa,
Ushuru wa Bidhaa na Mapato yasiyo ya kodi yatokanayo na Mambo ya Muungano.
Kwa Rasimu kupendekeza muundo wa Serikali tatu na kuipa Serikali ya Muungano
majukumu ambayo haina mamlaka nayo, ni kuzusha utata na migongano kati ya
Serikali ya Muungano na nchi washirika. Mkichagua mfumo wa Serikali tatu,
inawalazimu muyaondoe mambo hayo kwani Serikali ya Muungano haistahili
kuyatekeleza na wala haina uwezo wa kuweka masharti kwa Serikali za nchi
washirika kwa mambo yaliyo kwenye mamlaka ya nchi hizo. Lakini kama mtaamua
tuendelee na muundo wa Serikali mbili, mambo haya mazuri yanatekelezeka na
Serikali ya Muungano bila ya matatizo. Katika uandishi wa Rasimu Utumishi
katika Serikali ya Muungano haumo katika Orodha ya Mambo ya Muungano. Ni lazima
liwemo. Hayo ni baadhi tu ya masuala yahusuyo uandishi katika Rasimu. Naamini
mkiisoma Rasimu kwa makini mnaweza kuyagundua mengineyo.
Dhana Mpya
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Katika Rasimu kuna dhana mpya na mambo mapya kadhaa yaliyoingizwa ambayo
yanabadili utaratibu wa sasa wa uendeshaji wa nchi na mambo mbalimbali. Nawaomba
mfanye uchambuzi wa kina kwa kila kinachopendekezwa na kujiridhisha kuhusu
kufaa kwake na manufaa yake. Fanyeni hivyo ili tujihakikishie kuwepo kwa mambo
mazuri na uendeshaji mzuri wa shughuli katika taifa letu changa.
Mambo ni mengi na kwa ufinyu wa muda sitaweza kuyazungumzia yote. Niruhusuni
nizungumzie baadhi ya dhana na mambo mapya yaliyomo katika Rasimu. Jambo la
kwanza, kwa mfano, linahusu Ibara ya 128 (2)(d) inayoleta dhana ya “Mbunge
kupoteza Ubunge iwapo atashindwa kufanya kazi za Mbunge kwa miezi sita
mfululizo kutokana na maradhi au kizuizi ndani ya gereza”.
Watu hawana tatizo na Mbunge kuwa kizuizini ndani ya gereza kama amepatikana na
hatia Mahakamani na kuhukumiwa kifungo. Lakini, isijekuwa yuko rumande kwa
tuhuma akisubiri kesi kusikilizwa. Je akija kuonekana hana hatia na kuachiliwa?
Naungana na wale wanaoshauri kuwa jambo hili lifafanuliwe vizuri na kutambua
Mbunge kutiwa hatiani na kupata adhabu ya kifungo cha kipindi hicho. Ni bora
ifanyike hivyo sasa ili kuondoa mikanganyiko. Hakuna haja ya kusubiri mpaka
jambo hili lije kufafanuliwa baadaye kwa Sheria itakayotungwa na Bunge.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Kwa upande wa mtu kupoteza Ubunge kwa sababu ya “kuugua kwa miezi sita
mfululizo” ni maoni ya watu wengi kuwa huu ni ukatili ambao haustahili kufanywa
na Katiba. Kuugua ndiyo ubinadamu na wakati mwingine Mbunge anaweza kupata
ajali akiwatumikia wananchi wa Jimbo lake. Anaweza kuugua kwa miezi sita au
zaidi na kupona kabla ya kipindi chake cha Ubunge kufika mwisho. Kwa nini
awekewe ukomo wa miezi sita? Katiba ya mwaka 1977 tunayotumia sasa haina sharti
hilo. Watu wanauliza hoja na haja ya kuwa na sharti hili kwenye Katiba mpya ni
ipi? Wanasema kwa kweli anachostahili Mbunge huyu kufanyiwa ni kuuguzwa afya
yake iimarike ili aendelee kutumikia watu wake, na siyo kupoteza uongozi wake.
Tusiwatie watu kishawishi cha kukatiza matibabu ili kukwepa sharti hilo. Ni
vyema jambo hili mkalitazama kwa makini, na muone kama linastahili kuwepo au
hapana.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Katika Rasimu hii imeingizwa dhana mpya ya kuweka ukomo wa vipindi vitatu kwa
Wabunge. Tena mapendekezo haya hayasemi vipindi vitatu mfululizo au la!. Jambo
hilo limezua mjadala motomoto katika jamii. Ni vizuri mkajiridhisha juu ya
sababu za msingi na manufaa ya kufanya hivyo hapa Tanzania. Mazoea yetu na ya
kwingineko duniani ni kuweka ukomo kwa Wakuu wa Nchi kwa sababu nzuri na rahisi
kuzielezea. Lakini, kuwawekea ukomo Wabunge ni jambo jipya na huenda Tanzania
tukawa wa kwanza. Nashawishika kuungana na wale wanaopendekeza kuwa pengine ni
mapema mno kuanzisha utaratibu huo hapa kwetu.
Nachelea kuwa tutainyima nchi yetu fursa ya kupata watu wenye maarifa na uzoefu
mzuri wa uongozi kwa nafasi ya Ubunge au kwa nafasi za uongozi wa Taifa bila ya
sababu za msingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Jambo lingine jipya linalopendekezwa na Tume ni utaratibu wa kumuondoa Mbunge
katikati ya kipindi chake cha uongozi. Kwa hoja linaonekana kuwa jambo jema
lakini naomba athari zake mzitafakari vizuri. Kuna hatari ya kuanzisha
misuguano kwenye Majimbo na kuwaacha Wabunge wasifanye kazi zao kwa utulivu
bali wawe wanajihami dhidi ya wapinzani wao kuwatengenezea fitna za kuwatoa.
Utaratibu unaopendekezwa wa Chama chake kujaza nafasi ya Mbunge inapokuwa wazi
katika mazingira hayo nao unaweza kuwa ndicho kichocheo kikubwa cha vuguvugu la
kumuondoa Mbunge. Walioshindwa kwenye kura ya maoni wanaweza kufanya kazi ya
kuwachimba wenzao mpaka waondoke. Jipeni muda wa kupima faida na hasa thamani
inayoongezwa na kuanzisha utaratibu huo. Naomba tujiridhishe kama jambo hili
jipya lina tija. Hivi kupewa nafasi kila miaka mitano kurudi kwa wananchi
hakutoshi kumuondoa Mbunge ambaye watu wamemchoka?
Muundo wa Muungano
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Jambo lingine kubwa lililopendekezwa na Tume ambalo limevuta hisia za karibu
watu wote nchini linahusu muundo wa Muungano wetu kuwa wa Serikali tatu badala
ya mbili za sasa. Pendekezo hili limezua mjadala mkubwa tangu lilipotolewa
katika Rasimu ya kwanza na kurudiwa katika Rasimu ya pili. Wakati mwingine
mjadala umekuwa mkali na wa hisia kali kwa kila upande.
Kwa kweli hili ndilo jambo kubwa kuliko yote katika Rasimu kwa sababu
linapendekeza kuanzishwa kwa muundo na mfumo mpya wa kuendesha nchi yetu. Hii
ndiyo agenda mama ya Bunge hili ambayo kila Mtanzania anasubiri kwa hamu uamuzi
wenu utakuwa upi. Ombi langu kwenu ni kuwa watulivu mnapojadili suala hili.
Epukeni jazba ili mfanye uamuzi ulio sahihi. Lazima mtambue uamuzi usiokuwa
sahihi kwa jambo hili una hasara kubwa. Tunaweza kupoteza kitu tulichokijenga
kwa gharama kubwa kwa nusu karne iliyopita. Tanzania inaweza kuwa nchi iliyojaa
migogoro na matatizo mengi ambayo hatunayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wajumbe;
Kama alivyoeleza Mwenyekiti wa Tume Mheshimiwa Jaji Joseph Sinde Warioba, mara
kadhaa, mjadala au madai ya kutaka muundo wa Serikali tatu si jambo jipya.
Ulikuwepo hata wakati wa mazungumzo ya kuunganisha nchi zetu mbili mwaka 1964.
Ulikuwa kiini cha kuchafuka kwa hali ya hewa ya kisiasa Zanzibar mwaka 1984.
Muundo huu uliwahi kupendekezwa na Tume ya Nyalali mwaka 1992, ndiyo hoja ya
G55 mwaka 1993 na umependekezwa pia na Tume ya Jaji Kisanga ya mwaka 1998.
Lakini mara zote hizo mapendekezo hayo hayakukubaliwa.
Waasisi wa taifa letu, yaani Mwalimu Julius Nyerere, aliyekuwa Rais wa Jamhuri
ya Tanganyika wakati ule na Sheikh Abeid Amani Karume, aliyekuwa Rais wa
Jamhuri ya Watu wa Zanzibar wakati ule, waliamua kuchagua Muungano wa Serikali
mbili tulionao sasa. Walitoa sababu mbili kuu: “ni muundo unaoihakikishia
Zanzibar kuwa haimezwi na Tanganyika; na pia unaiepusha Tanganyika kubeba mzigo
mkubwa wa kugharamia Serikali ya Tanganyika na ile ya Muungano”.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Natambua kuwepo kwa rai ya kutaka Mwalimu Nyerere asitumiwe katika mjadala huu.
Nionavyo mimi ni vigumu kuacha kujadili fikra za Mwalimu Nyerere na Sheikh
Karume katika jambo hili. Wao ndiyo wa mwanzo kujadili na kukubaliana kuwa
mfumo wa Serikali mbili ndiyo bora kwa nchi yetu. Iweje leo tunapozungumzia
kuubadili, mawazo yao yawe hayafai kutumika au hata kuzungumzwa. Hivi hasa
mawazo ya nani pekee ndiyo bora zaidi kutumika? Tutakuwa hatuutendei haki
mjadala huu na sisi wenyewe tunaoshiriki katika mchakato huu. Rai yangu kwenu
ni kuwa mzitazame hoja zote kwa marefu na mapana yake ili mpime kama zipo
sababu za kuubadili muundo wa sasa wa Muungano wa Serikali mbili na kuleta wa
Serikali tatu. Na, kama zipo mabadiliko hayo yaweje! Lazima mfanye uamuzi kwa
utambuzi na hoja zenye mashiko. (you must make an informed decision).
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Tume imetoa sababu mbili kubwa za kupendekeza muundo wa Serikali tatu. Sababu
ya kwanza ni kwamba ndiyo matakwa ya Watanzania wengi kote Zanzibar na Tanzania
Bara. Inaeleza kuwa idadi kubwa ya Watanzania waliotoa maoni, yaani asilimia
60.2 wa kutoka Zanzibar wanaunga mkono muundo wa Serikali ya Mkataba, na
asilimia 61.3 wa kutoka Tanzania Bara wanaunga mkono muundo wa Serikali tatu.
Sababu ya pili ni kwamba muundo huo unatoa majawabu ya uhakika na endelevu kwa
changamoto za muundo wa sasa wa Serikali mbili zinazonung’unikiwa na watu wa
pande zetu mbili za Muungano.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Sababu hizi mbili kuu zilizotolewa na Tume zimezua mjadala mkali katika jamii.
Wapo wanaokubaliana na Tume na wapo wasiokubaliana nayo. Wapo wanaosema Tume
imesema kweli kwamba Watanzania wengi wanaunga mkono muundo wa Serikali tatu,
hivyo muundo wa Serikali tatu hauepukiki. Ndiyo matakwa ya wengi hivyo msemo wa
Kiswahili usemao wengi wape uheshimiwe.
Lakini wapo wanaodai kuwa takwimu za Tume hazionyeshi ukweli huo. Wanasema kuwa
taarifa ya Tume imeonesha kuwa Watanzania waliotoa maoni yao kwa Tume kwa mdomo
na maandishi walikuwa 351,664. Kati yao ni wananchi 47,820 au sawa na asilimia
13.6 ndiyo waliokerwa na muundo wa Muungano hivyo wakauzungumzia. Wananchi
303,844 au sawa na asilimia 86.4 muundo wa Muungano kwao halikuwa tatizo, ndiyo
maana hawakuuzungumzia kabisa. Wanahoji kuwa iweje leo asilimia 13.6 ya
Watanzania wote waliotoa maoni wageuke kuwa ndiyo Watanzania walio wengi!
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Wanasema pia, kwamba mbona Taarifa ya Tume yenyewe, kuhusu takwimu (uk. 66 na
67), inaonesha kwamba kati ya hao watu 47,820 waliotoa maoni kuhusu Muungano,
ni watu 17,280 tu ambao ni sawa na asilimia 37.2 ndiyo waliotaka muundo wa
Serikali tatu, asilimia 29.8 walitaka Serikali mbili, asilimia 25.3
walipendekeza Serikali ya Mkataba na asilimia 7.7 walipendekeza Serikali moja.
Hii hoja ya Watanzania wengi kutaka Serikali tatu msingi wake upi?
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Takwimu za Tume (uk. 57) zinaonyesha, vilevile kuwa Tume ilipokea maoni
772,211. Kati ya hayo asilimia 10.4 tu ndiyo yaliyozungumzia muundo wa Muungano
na asilimia 88.6 hayakuzungumzia Muungano bali mambo mengine. Hivyo basi
wanahoji pia kwamba kama muundo wa Muungano ungekuwa ni jambo linalowakera
Watanzania wengi, lingedhihirika kwenye idadi ya watu waliotoa maoni na kwenye
idadi ya maoni yaliyotolewa. Yote hayo hayakujitokeza. Waliouzungumzia Muungano
walikuwa asilimia 13.6 tu ya watu wote waliotoa maoni na maoni yanayohusu
Muungano yalikuwa asilimia 10.4 ya maoni yote. Hivyo basi, wanauliza “usahihi
wa hoja ya Watanzania wengi kutaka Serikali tatu uko wapi?”
Changamoto za Muundo wa Serikali Mbili
Mheshimiwa Mwenyekiti na Waheshimiwa Wajumbe;
Kama nilivyokwishagusia awali, sababu ya pili ambayo Tume inatoa kuhusu kufaa
kwa muundo wa Serikali tatu ni kwamba mfumo huu unajibu changamoto nyingi za
muundo wa Serikali mbili. Tume imeainisha vizuri changamoto za muundo wa
Serikali mbili. Kwa upande wa Zanzibar wanalalamikia kile kinachoitwa Tanzania
Bara kuvaa koti la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na hivyo kutumia mamlaka ya
Serikali ya Muungano kujinufaisha yenyewe. Fursa hiyo Zanzibar hainayo. Aidha,
wanasema mipaka na mamlaka ya Serikali ya Muungano kwa mambo ya Muungano, na
kwa mambo ya Tanzania Bara haijaainishwa vizuri ikaeleweka. Wazanzibari pia,
wanazungumzia mkanganyiko kuhusu ugawanaji wa mapato, na jinsi ya kuchangia
shughuli za Muungano baina ya Serikali ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar. Vilevile, wanalalamikia Rais wa Zanzibar kuondolewa kuwa Makamu wa
Rais wa Jamhuri ya Muungano.
Aidha, kuna malalamiko kuwa orodha ya mambo ya Muungano iliyoongezwa kutoka
mambo 11 mwaka 1964 mpaka 22 mwaka 1992 imepunguza uhuru wa Zanzibar kwa mambo
yake ya ndani.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Kwa upande wa Tanzania Bara, Tume inaeleza kuwepo kwa manung’uniko kuwa
Muungano wa Serikali mbili umepoteza utambulisho wa kihistoria wa Tanganyika na
fursa ya watu wa upande wa Tanzania Bara kutetea maslahi yao ndani ya Muungano.
Wanasema Zanzibar sasa imekuwa nchi huru; ina bendera yake, wimbo wake wa taifa
na Serikali yake. Aidha, wanasema Zanzibar imebadili Katiba na kujitambulisha
kama nchi na kuchukua madaraka ya Bunge la Muungano, kwa vile Sheria
zinazotungwa na Bunge lazima zipelekwe kwenye Baraza la Wawakilishi kupata kibali
cha kutumika Zanzibar. Wananchi wa Tanzania Bara pia wanalalamikia kutokuwa na
haki ya kumiliki ardhi Zanzibar wakati wenzao wa kutoka Zanzibar wanayo haki
hiyo Tanzania Bara. Na wao vilevile wananung’unikia mkanganyiko kuhusu ugawaji
wa mapato na jinsi ya kuchangia gharama za uendeshaji wa shughuli za Muungano
baina ya Serikali ya Muungano na Serikali ya Zanzibar. Hizi ndizo baadhi ya
changamoto ambazo Tume inaona jawabu lake ili kuzitanzua ni kubadili muundo wa
Muungano kuwa wa Serikali tatu badala ya mbili za sasa.
Faida za Muundo wa Serikali Tatu
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Tume ya Mabadiliko ya Katiba imefafanua kwamba mfumo wa Serikali tatu
utagawanya vizuri madaraka kati ya mamlaka tatu za Muungano. Unawezesha
Washirika wa Muungano kubaki na utambulisho wao wa kihistoria na kiutamaduni na
hivyo, utawezesha kuondoa hisia za Zanzibar kumezwa na Muungano. Pia unawezesha
kila upande wa Tanzania kuendesha mambo yake yasiyo ya Muungano kadri
wanavyoona inafaa. Vile vile unaweza ukaleta ushindani wa kimaendeleo baina ya
washirika na hivyo kusaidia kukuza maendeleo ya nchi.
Faida za Muundo wa Serikali Mbili
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Pamoja na kuainisha changamoto za muundo wa Serikali mbili na kupendekeza kuwa
muundo wa Serikali tatu ndio utakaosaidia kuzitatua, Tume haikuacha kutambua
manufaa na mchango muhimu uliotolewa na muundo wa Serikali mbili kwa nchi yetu.
Tume inasema kuwa muundo wa Serikali mbili unapunguza gharama za uendeshaji wa
shughuli za umma. Umesaidia kujenga uhusiano na ushirikiano mzuri katika nyanja
mbalimbali baina ya wananchi wa pande zetu mbili za Muungano. Umezuia mkubwa
kummeza mdogo; na umedumisha Muungano mpaka kuufikisha hapa ulipo tangu
kuasisiwa kwake takriban miaka 50 iliyopita (1964). Aidha, umesaidia kudumisha
amani, umoja na utulivu hapa nchini.
Changamoto za Muundo wa Serikali Tatu
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Pamoja na kuelezea ubora wa muundo wa Serikali tatu kama jawabu kwa changamoto
za Serikali mbili, Tume inakiri kuwa hata muundo huu nao una changamoto zake.
Kwanza kabisa, Taarifa ya Tume inaeleza kuwa kutakuwa na gharama kubwa za
uendeshaji wa shughuli za umma. Mheshimiwa Jaji Joseph Warioba alitutoa hofu
kuhusu gharama ingawaje mwaka 1993, Mwalimu alikuwa na mawazo tofauti. Alisema
kwamba: “watu …wanaodhani kuwa gharama ya Serikali yo yote kati ya hizo
ingekuwa ndogo, (Waulizeni Wazanzibari) na wala gharama ya Serikali ya
Shirikisho isingekuwa ndogo hata bila gharama ya mambo yasiyo ya Shirikisho”.
Ni matumaini yangu kwamba katika mjadala wenu mtajipa nafasi ya kulitafakari
suala hili kubwa na nyeti.
Tume imesema pia kwamba, Muundo huu, unaweza kuibua tatizo la uchangiaji wa
gharama za uendeshaji wa shughuli za umma baina ya nchi washirika. Vilevile,
kuna uwezekano wa kuwepo sera zinazokinzana au kutofautiana juu ya masuala ya
msingi ya nchi na kuzua mgogoro kati ya washirika wa Muungano na baina ya nchi
washirika na Serikali ya Muungano. Aidha, upo uwezekano mkubwa kwa muundo huu
kuleta tofauti za kimaendeleo baina ya pande mbili za Muungano kutokana na kila
upande kuwa na sera na mipango tofauti.
Tume pia imeelezea hatari ya muundo wa Serikali tatu kukuza hisia za utaifa
(nationalistic feelings) kwa nchi washirika, hivyo kuweza kudhoofisha Muungano.
Muundo huu pia unaweza kuleta misuguano (paralysis and deadklocs in decision
making) katika kufanya uamuzi juu ya masuala muhimu ya kitaifa. Changamoto hizo
si tu zinaweza kuwa tishio kwa ustawi wa Muungano bali pia hata uhai wake. Kwa
ajili hiyo kuchagua muundo wa Serikali tatu kuna maana ya kufanya kazi ya ziada
ya kuzikabili changamoto hizi ili zisiue Muungano wenyewe. Changamoto ambazo si
ndogo hata kidogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Wanaounga mkono muundo wa Serikali mbili wanasema kuwa kwa mlolongo huu wa
changamoto zilizoainishwa na Tume yenyewe, unadhihirisha kuwa muundo wa
Serikali tatu hautapunguza matatizo ya Muungano wetu bali utayaongeza maradufu
kuliko ilivyo sasa. Wanakiri kuwepo kwa changamoto katika muundo wa sasa wa
Muungano. Hata hivyo, wanaamini zinaweza kushugulikiwa na kupatiwa ufumbuzi
bila ya kuhitaji kuwa na Serikali ya tatu. Wanatoa mifano kadhaa ya jinsi
Serikali zetu zilivyoshughulikia changamoto za Muungano katika kipindi cha uhai
wake na mafanikio yaliyopatikana.
Katika kushughulikia kero za Muungano, Serikali zetu mbili ziliunda Tume ya
Shelukindo mwaka 1992 na Kamati ya Pamoja ya Serikali zetu mbili mwaka 1993.
Mambo mengi yaliyoainishwa katika Tume ya Shelukindo na Kamati ya Pamoja
yameshughulikiwa na kupatiwa ufumbuzi. Kwa upande wa kero zilizoelezwa kwenye
Tume ya Shelukindo, ilipofikia mwaka 2006 yalikuwa yamebakia mambo 13 kati ya
31. Kwa jumla, kwa kero zilizoibuliwa na Tume ya Shelukindo na Kamati ya
Pamoja, hivi sasa yamesalia mambo sita tu. Kimsingi ni mambo yahusuyo maslahi
ya kiuchumi na yote yapo katika hatua nzuri za kuyamaliza. Mambo hayo ni:
1. Mgawanyo wa mapato:
(a) Hisa za SMZ zilizokuwa katika Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki
(b) Mgawanyo wa Mapato yatokanayo na faida ya Benki Kuu.
2. Utafutaji na uchimbaji mafuta na gesi asili.
3. Ushirikiano wa Zanzibar na taasisi za nje.
4. Ajira kwa watumishi wa Zanzibar katika taasisi za Muungano.
5. Usajili wa vyombo vya moto.
6. Tume ya Pamoja ya Fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Serikali zetu mbili zimeamua kwa dhati kutumia fursa ya mchakato huu wa
mabadiliko ya Katiba kuyamaliza yale yanayohitaji kuingizwa kwenye Katiba ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mambo hayo ni matatu yafuatayo:
1. Utafutaji na uchimbaji mafuta na gesi asili.
2. Ushirikiano wa Zanzibar na taasisi za nje.
3. Tume ya Pamoja ya Fedha.
Matatu mengine yatamalizwa kwa kutumia taratibu za kiutawala.
Hali kadhalika, katika kipindi cha mpito kinachopendekezwa na Tume yaani 2015 –
2018 ni nafasi nzuri ya kushughulikia masuala yenye migongano kati ya Katiba ya
Zanzibar na ile ya Jamhuri ya Muungano. Mimi naishi kwa matumaini na kwa vile
tunayo dhamira njema ya kuimarisha Muungano wetu, naamini tutaweza kuziondoa
tofauti zilizopo.
Orodha ya Mambo ya Muungano
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Kuhusu orodha ya mambo ya Muungano kuwa 22 badala ya 11 ya awali, napenda
kuwahakikishia kuwa Serikali ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
hazina kigugumizi wala upungufu wa dhamira ya kisiasa ya kuyapunguza yale
yanayopunguzika. Napenda kwanza kabisa, ieleweke kuwa kilichoongeza orodha hiyo
si hila za Serikali ya Muungano kutaka kupunguza madaraka ya Zanzibar kwa mambo
yake ya ndani. Na, wala siyo udhaifu wa viongozi wa Zanzibar katika kutetea
maslahi ya nchi yao. La hasha.
Pili, naomba ieleweke kuwa, kila kilichoongezwa katika Orodha ya Mambo ya
Muungano kilikuwa na sababu inayoeleweka, inayoelezeka na iliyokubalika na
pande zote mbili za Muungano. Hakuna hata jambo moja lililoingizwa kwenye
Katiba kwa kificho. Taratibu stahiki za kikatiba na kisheria zilifuatwa. Hoja
ziliwasilishwa Bungeni na kujadiliwa kwa uwazi na uamuzi ulifanywa na Bunge kwa
kuzingatia kanuni ya theluthi mbili ya kura za kila upande wa Muungano.
Kumbukumbu zipo katika Hansard za Bunge la Muungano, ambazo ziko wazi kwa kila
mtu anayetaka kuzisoma asome. Nashauri mkazisome ili mpate kujua ukweli na
undani wa kila kilichoongezwa na sababu za kufanya hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Nchi zetu mbili zilipoungana mwaka 1964 na kuzaa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, kulikuwa na mambo 11 kwenye Orodha ya Mambo ya Muungano. Mambo hayo
ni haya yafuatayo:
1. Katiba ya Jamhuri ya Muungano,
2. Mambo ya Nje,
3. Ulinzi,
4. Polisi,
5. Hali ya Hatari,
6. Uraia,
7. Uhamiaji,
8. Biashara ya nje na mikopo,
9. Utumishi katika Serikali ya Muungano,
10. Kodi ya Mapato, Kodi ya Makampuni, Ushuru wa Forodha na Ushuru wa Bidhaa,
11. Bandari, Mambo ya Anga, Posta na Simu.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Kati ya mwaka 1965 na 1992 mambo ya Muungano yaliongezeka kutoka 11 hadi
kufikia 22, kimsingi kutokana na mambo mbalimbali yaliyotokea nchini na kwenye
ukanda wetu wa Afrika Mashariki. Pande zetu mbili za Muungano zilikubaliana
kuwa mambo hayo yaongezwe katika Katiba na taratibu za kisheria na Kikatiba
zilifuatwa. Kwa idhini yako naomba nitoe maelezo kwa ufupi kwa yale
yaliyoongezwa na kitu kilichosababisha mabadiliko hayo kufanywa.
1. Jambo la kwanza kuongezwa, yaani la 12 lilikuwa ni “sarafu, mabenki na fedha
za kigeni”. Hii ilifanyika tarehe 10 Juni, 1965 kufuatia kuvunjika kwa Bodi ya
Sarafu ya Afrika Mashariki (East African Currency Board) mwaka 1964. Kwa ajili
hiyo, kila nchi mwanachama wa Jumuiya ililazimika kuwa na sarafu yake na
mipango yake ya kusimamia mambo yake ya kibenki na fedha. Serikali zetu mbili
zilikubaliana masuala hayo yashughulikiwe na Serikali ya Muungano na Muswada
husika wa Bunge uliidhinishwa kuwa Sheria na Mzee Abeid Amani Karume aliyekuwa
akikaimu Urais tarehe 10 Juni, 1965.
2. Tarehe 11 Agosti, 1967 yaliongezwa mambo yafuatayo kwenye
Orodha ya Mambo ya Muungano:-
(a) Leseni za Viwanda na Takwimu, (Jambo la 13)
(b) Elimu ya Juu, (Jambo la 14)
(c) Jambo la 15 lilikuwa ni mambo yote yaliyokuwa kwenye Nyongeza ya 10 ya
Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Nyongeza hiyo ilikuwa na mambo 27
ambayo Serikali ya Muungano ilipewa jukumu la uratibu. Mambo hayo ni pamoja na
Mahakama ya Rufani ya Afrika Mashariki, Utabiri wa Hali ya Hewa, Utafiti,
Vipimo na Mizani, Huduma ya Usafiri wa Reli, Barabara, Usafiri wa Majini na
kadhalika.
3. Tarehe 22 Julai, 1968 “rasilimali ya mafuta, petroli na gesi
asilia” iliongezwa kwenye Orodha ya Mambo ya Muungano na kuwa jambo la 16.
Kimsingi Serikali ya Muungano ilipewa jukumu la kuagiza mafuta ya petroli na
gesi asilia kwa ajili ya nchi nzima. Baada ya kupanga upya Orodha ya Mambo ya
Muungano, suala la rasilimali ya mafuta likawa la 15.
4. Tarehe 22 Novemba, 1973 Baraza la Mitihani la Taifa
liliongezwa na kuwa jambo la 16. Hii ilifuatia kuvunjika kwa Baraza la Mitihani
la Afrika Mashariki mwaka 1971 na hivyo nchi yetu kulazimika kuunda Baraza la
Mitihani la Taifa mwaka 1973.
5. Mwaka 1984 yalipofanyika mabadiliko makubwa katika Katiba ya
mwaka 1977, Orodha ya Mambo ya Muungano ilipangwa upya. Mambo yaliyokuwemo
kwenye Nyongeza ya 10 ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na kuorodheshwa kama Jambo
la 15 katika Orodha ya Mambo ya Muungano yalipunguzwa na kubaki matano. Mambo
hayo yalipewa namba kama ifatavyo:- Usafirishaji wa Anga kuwa Jambo la 17,
Utafiti kuwa la 18, Utabiri wa Hali ya Hewa kuwa la 19 na Takwimu kuwa la 20 na
Mahakama ya Rufani ya Tanzania ikawa jambo la 21.
6. Tarehe 17 Mei, 1992 likaongezwa jambo la “Uandikishaji wa Vyama
vya Siasa” na kuwa jambo la 22. Hii ilifuatia kuanzishwa kwa Mfumo wa Vyama
Vingi vya Siasa na hasa uamuzi kuwa vyama vitakuwa vya kitaifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Bila ya shaka maelezo haya yatasaidia kuelezea nini kimeongezwa na mazingira ya
kuongezwa kwake ni yepi. Kulikuwepo na sababu za msingi na wala siyo hila ya
namna yo yote ile iliyofanywa na mtu ye yote mwenye nia mbaya na Zanzibar. Kama
tulivyoona mambo mengi yalihusu kilichokuwa kinatokea ndani ya Jumuiya ya
Afrika Mashariki. Kila yalipotokea mabadiliko katika uendeshaji wa shughuli za
Jumuiya ya Afrika Mashariki, huduma zilizokuwa zikitolewa na Jumuiya
zilikabidhiwa Serikali ya Muungano kubeba kwa sababu ya uwezo wake mkubwa wa
kiuchumi. Yale yaliyokuwa yanagusa sehemu zetu mbili za Muungano yaliingizwa
katika Orodha ya Mambo ya Muungano. Mengineyo yaliachiwa kila upande
kushughulikia ilivyoona inafaa. Kwa maana hii basi, mambo ambayo yalitokana na
uamuzi wetu wenyewe ni mawili tu. Mambo hayo ni rasimali ya mafuta na gesi
asilia (1968), na uandikishaji wa vyama vya siasa (1992).
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Ni msimamo wa Serikali zetu mbili, tangu mwanzo mpaka leo kwamba, iwapo
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeshajenga uwezo wake wa kufanya baadhi ya
mambo katika Orodha ya Mambo ya Muungano ipewe uhuru wa kufanya hivyo. Lililo
muhimu ni kuwa zisiondolewe tunu zenyewe za Muungano wetu. Ndiyo maana, mambo
kama vile bandari, takwimu, kodi ya mapato, leseni za biashara, utafiti na
mengineyo, yanasimamiwa na kuendeshwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
pamoja na kuwemo kwenye Orodha ya Mambo ya Muungano. Imekuwa hivyo kwa miaka
kadhaa sasa na imethibitika kuwa Zanzibar inayamudu. Ni makusudio yetu kutumia
fursa ya mchakato huu sasa kuyaondoa rasmi mambo hayo na mengineyo
tutakayokubaliana kutoka kwenye Orodha ya Mambo ya Muungano.
Rasilimali ya Mafuta na Gesi Asilia
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Kwa ajili hiyo tumekubaliana kuliondoa suala la rasilimali ya mafuta na gesi
asilia lisiwe jambo la Muungano. Jambo hili tulishakubaliana tangu wakati wa
Rais Amani Abeid Karume tuliondoe na hata alipokuja Rais Shein msimamo
haukubadilika. Kilichotuchelewesha kutekeleza ni kuibuka kwa fikra za kuwa na
mchakato huu wa Katiba mpya. Tuliona kuwasilisha Bungeni Muswada wa Sheria wa
kuondoa jambo hili katikati ya mchakato huu, ingeweza kuzua matatizo yasiyokuwa
ya lazima. Tungeulizwa haraka ni ya nini tungeweza kukosa majibu.
Hatimaye wakati wake wa kulimaliza suala hili sasa umefika. Misemo ya wahenga
ya “subira yavuta heri” na “kawia ufike” imetuongoza vyema tumefika mahali
tunaweza kufanya hivyo. Zipo sababu mbili zilizotushawishi kuamua kuitoa
rasilimali hii kwenye Orodha ya Mambo ya Muungano. Kwanza kwamba, siku hizi
Serikali haiagizi mafuta. Kazi hiyo hufanywa na makampuni binafsi. Pili,
kwamba, rasilimali ya mafuta na gesi yakipatikana Zanzibar ni suala la kiuchumi
ambalo lipo kwenye mamlaka ya Zanzibar kama ilivyo karafuu, hiliki, mwani na
kadhalika. Au kama ilivyo dhahabu, gesi, pamba, kahawa na kadhalika kwa upande
wa Tanzania Bara. Hivyo, Zanzibar iachwe kumiliki rasilimali yake ya kiuchumi.
Zanzibar na Ushirikiano wa Kimataifa
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Jambo lingine muhimu ambalo Serikali zetu mbili zimelizungumza na kukubaliana
tulitafutie ufumbuzi ni kuhusu Zanzibar kupata fursa ya kujiunga na mashirika
ya kimataifa, kukopa na kupata misaada kutoka nchi za nje bila kizuizi. Kwa
sasa fursa hiyo ina vikwazo vya namna mbalimbali. Ni ukweli usiopingika kuwa
jambo hili limechangia kwa kiasi kikubwa kujenga hisia hasi kuhusu Muungano kwa
upande wa Zanzibar. Aidha, limechangia sana kuchafua hali ya hewa ya kisiasa
Zanzibar kwa nyakati mbalimbali. Hata zile kauli kwamba Tanzania Bara
imejificha kwenye koti la Serikali ya Muungano, na kutaka itoke ionekane ili
iache kunufaika isivyostahili, zinazochangiwa sana na mazingira haya iliyonayo
Zanzibar. Serikali zetu mbili zinaamini kuwa mambo haya yakipatiwa ufumbuzi
tutakuwa tumeondoa kizingiti kikubwa katika ustawi wa Muungano wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
tumekubaliana kuwa, tutumie fursa za mchakato huu kuyamaliza mambo haya yaishe!
Bahati nzuri dhana iliyopo katika Ibara ya 65(2) ya Rasimu inatoa jawabu
mwafaka kwa tatizo hili. Tukikubaliana, itaipa Zanzibar “uwezo na uhuru wa
kuanzisha uhusiano na ushirikiano na jumuiya au taasisi yo yote ya kikanda na
kimataifa kwa mambo yaliyo chini ya mamlaka yake kwa mujibu wa Katiba ya nchi”
bila kizuizi. Ni maoni ya Serikali zetu mbili kuwa fursa hiyo inaweza kutolewa
kwa Zanzibar bila ya kulazimika kuwa na muundo wa Serikali tatu. Hatuuoni
ulazima huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Kwa maoni yangu kitu kingine muhimu cha kufanya ni kuongeza msukumo,
utakaohakikisha kuwa Tume ya Pamoja ya Fedha inatimiza ipasavyo majukumu yake.
Wanaohusika na utekelezaji wa maamuzi yake wabanwe ipasavyo kutimiza wajibu
wao. Iwekwe mifumo na masharti katika sheria au Katiba ya kuwabana watekelezaji
kwa ajili hiyo. Hali kadhalika ihakikishwe kuwa, Akaunti ya Pamoja inaanzishwa
bila ajizi na kutumika na pande zote. Aidha, mfumo wa mawasiliano na
ushirikiano baina ya Serikali zetu mbili yaani Kamati ya Pamoja ya Serikali ya
Muungano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, upewe nguvu ya kisheria na kama
hapana budi upewe nguvu ya Kikatiba. Tukifanya hivyo tutafanikiwa kuyaweka
mambo yote sawa hata bila ya kuhitaji kuunda Serikali ya tatu.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Waheshimiwa Wajumbe;
Katika mjadala kuhusu mapendekezo ya kuwa na muundo wa Muungano wenye Serikali
tatu, wananchi wametoa maoni na mapendekezo mengi mazuri kuhusu changamoto za
Serikali tatu zilizoainishwa na Tume na namna ya kuzitatua. Tena yapo maoni ya
watu wanaopenda muundo wa Serikali tatu na wasiopenda muundo wa Serikali tatu.
Nawaomba myatafakari kwa uzito unaostahili. Yapo mambo muhimu ya kuyatafutia
ufumbuzi. Kwanza, kwa mfano ni ile hoja kwamba Serikali ya Muungano
inayopendekezwa haikujengeka kwenye msingi imara. Haina nguvu yake yenyewe za
kusimama. Inategemea mno ihsani ya nchi washirika. Kwa sababu hiyo inaweza
kuanguka wakati wowote, na Muungano kusambaratika, iwapo itakosa ihsani ya nchi
washirika. Tena inaweza kuwa hivyo hata kama ni mmoja wa washirika amefanya
hivyo.
Pili, kwamba, haielekei Serikali hiyo ina chanzo cha uhakika cha mapato ya
kuiwezesha kusimama yenyewe na kutekeleza majukumu yake. Ushuru wa bidhaa
unaopendekezwa unatiliwa shaka kuwa hautatosheleza mahitaji. Pia, kwamba,
hakuna uhakika wa fedha hizo kupatikana kwa vile, Serikali ya Muungano haina
chombo chake chenyewe cha kukusanya mapato hayo. Itategemea vyombo vya nchi
washirika kuikusanyia na kuipelekea. Kuna hatari ya shughuli za Serikali ya
Muungano kusimama wakati wo wote au hata kusimama kabisa kwa sababu ya nchi
washirika kuchelewa au kushindwa kuwasilisha makusanyo ya kutoka kwao.
Bahati mbaya Serikali ya Muungano haina uwezo wala nyenzo za kuhakikisha kuwa
mapato yake yanawasilishwa. Serikali hiyo haina mamlaka ya kuzibana nchi
washirika kuwasilisha au kuziwajibisha zisipofanya hivyo. Katika mazingira hayo
ni rahisi kwa Serikali ya Muungano kukwama na kushindwa kutekeleza majukumu
yake. Huu ni muundo ambao inakuwa ni rahisi sana kwa Muungano kuvunjika.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Katika Rasimu ya Katiba, Serikali ya Muungano inapewa fursa ya kukopa kama
chanzo cha kujipatia mapato ya kuendesha shughuli zake. Lakini, kwa sababu ya
kukosa rasilimali zake yenyewe, huenda ikawa vigumu kwa Serikali hiyo
kukopesheka. Kwa jumla hii ni Serikali ambayo ukuu wake hauna nguvu iliyo
thabiti, na watu wengine wanaona kama vile ukuu huo haupo kabisa. Akitokea
kiongozi ye yote wa nchi washirika akatunisha misuli dhidi ya Rais wa Muungano
au kupinga maamuzi ya Serikali au chombo cha Muungano, Rais na Serikali yake
watakuwa hawana lo lote la kufanya. Kwa kweli uhai wa Muungano katika muundo wa
Serikali tatu ni wa mashaka makubwa.
Hofu hizi kuhusu udhaifu wa Serikali ya Muungano chini ya mfumo wa Serikali
tatu unaopendekezwa, zinawasumbua hata wale wanaopendelea mfumo wa Serikali
tatu kuwepo. Wao wangependa iwepo Serikali ya Muungano yenye nguvu na inayoweza
kusimama yenyewe kwa kujitegemea. Wanaona kilichopendekezwa hakitoi matumaini
hayo. Hii ina maana kuwa lazima mawazo bora zaidi yatolewe ili kupata Serikali
ya tatu yenye ukuu unaoonekana na inayoweza kusimama yenyewe bila kuwa tegemezi
na egemezi kwa nchi washirika. Pia inaweza kuwa nguzo ya kutegemewa na nchi
washirika. Bila ya shaka Bunge hili likiamua tufuate mfumo huo linaweza
kuonyesha njia ya kuondoa hofu hizo. Kwa waumini wa Serikali mbili wanaona kuwa
huu ni uthibitisho wa ubora wa muundo wa Serikali mbili.
Changamoto za Hisia za Utaifa
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Katika kuainisha changamoto za muundo wa Serikali tatu, Tume ya Mabadiliko ya
Katiba imeyataja mambo mengine mawili makubwa ambayo ningependa Waheshimiwa
Wajumbe muyape tafakuri stahiki. Mambo hayo ni mosi, misuguano na mikwamo
(deadlocks and paralysis) katika kujadili na kufanya uamuzi kuhusu mambo muhimu
ya Muungano. Na pili, ni kuibuka kwa hisia za utaifa (nationalistic sentiments)
wa zamani kwa nchi washirika. Nawaomba myatafakari kwa makini sana mambo haya,
kwa sababu ya uwezo wake mkubwa wa kuhatarisha siyo tu ustawi na uhai wa
Muungano, bali hata usalama wa raia na mali zao. Naona hata Tume haikuweza
kupata ufumbuzi ulio mwafaka kabisa kwa changamoto hizi. Bila ya shaka katika
mijadala yenu Waheshimiwa Wajumbe mnaweza kusaidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Ni lazima lifanyike kila linalowezekana kuhakikisha kuwa maamuzi hayakwami
kwani yakikwama maana yake shughuli za Muungano zitakuwa zimekwama. Kama
hazitakwamuliwa kwa wakati ustawi wa Muungano utaathirika. Ikishindikana kabisa
kupatikana ufumbuzi Muungano unaweza kuvunjika. Kuibuka na kukua kwa hisia za
utaifa (nationalistic feelings) kwa nchi washirika, yaani Utanganyika na
Uzanzibari ni tishio kubwa sana kwa uhai wa Muungano. Hebu fikiria, watu
walioishi pamoja kidugu na kwa kushirikiana, kama watu wamoja na raia wa nchi
moja yaani Watanzania kwa miaka 50, kuja kujikuta uhusiano wao kuwa ni kati ya
Watanganyika na Wazanzibari na siyo kati ya Watanznaia. Kwa mujibu wa sensa
iliyopita takriban asilimia 90 ya Watanzania waliopo sasa wamezaliwa baada ya
mwaka 1964. Nchi wanayoijua ni Tanzania. Litakuwa ni jambo lenye mshtuko mkubwa
na athari zisizoweza kutabirika, watu hao watakapojikuta ni wageni wanaotakiwa
kutengenezewa utaratibu maalum wa kusafiri na kuishi wakiwa upande wa Muungano
ambao siyo kwao kwa asili. Wanakuwa wageni na fursa walizokuwa wanazipata
waendapo popote haiwi rahisi tena kuzipata.
Katika mazingira hayo ni rahisi sana chuki kupandikizwa na watu waliokuwa ndugu
mara moja watajikuta maadui. Aidha, watu wanaweza kujikuta wakilazimika kurudi
kwao kwa asili ama kwa kufukuzwa au kwa sababu ya mazingira kuwa magumu kiasi
cha kuona bora waondoke. Watu hao wanaweza kulazimika kuondoka huku wakiacha
nyuma kila kitu walichokichuma maishani.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Changamoto hizi kubwa mbili za mfumo wa Serikali tatu ambazo Tume imeziona, ni
za kweli. Si mambo ya kufikirika. Yale yaliyowakuta watu wenye asili ya
Tanzania Bara ya kuchomewa moto biashara zao Zanzibar mwaka 2012 na watu wenye
hisia kali za Uzanzibari, na kuwataka watu wa Bara waondoke Zanzibar, huenda
yakawa madogo. Matukio ya namna hii yanaweza kutokea pande zote mbili na
kusababisha maafa makubwa. Itaanza baina ya watu, baadaye itakuwa baina ya
Serikali zetu mbili na kuzifikisha nchi zetu mbili zilizokuwa ndugu na rafiki,
kwa nusu karne, ghafla kuwa maadui wasioombana chumvi na wasiotakiana heri.
Umoja wetu utatetereka na Muungano wetu unaweza kuvunjika. Kwa nini tufike
huko?
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Sisi viongozi tuliopewa dhamana ya kuamua kwa niaba ya wananchi wetu, hatuna
budi kuyapima mambo haya kwa umakini mkubwa ili tufanye uamuzi ulio sahihi.
Tusije tukajutia uamuzi wetu tutakapoona watu wanafukuzana, wanauana na mali
zao kuporwa. Na, tukifikia hatua hiyo Muungano kusambaratika halitakuwa jambo
la ajabu.
Kwa kweli, unapoyatafakari haya, ni rahisi kuelewa kwa nini wazee wetu waasisi
waliamua walivyoamua. Waliona mbali. Tusipuuze fikra zao na maono yao. Kuna
hatari ya nchi yetu na watu wake kupoteza kila kitu tulichokijenga kwa miaka
50. Badala ya kujenga tunaweza kujikuta tumebomoa hata msingi katika nchi
washirika. Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere mwaka 1993 alituasa kuhusu
hatari hiyo: “Hamuwezi kutenda dhambi kubwa namna hiyo bila adhabu… na adhabu
nyingine zimo mle mle ndani ya kitendo hazisubiri.”
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Siku moja kiongozi mmoja wa juu wa madhehebu ya dini nchini aliniuliza: “Hivi
Serikali mbili zikiwa na matatizo jawabu ni kuongeza ya tatu? Si matatizo ndiyo
yatazidi? Je, matatizo yakizielemea hizo Serikali tatu si kila mtu atachukua
njia yake? Mtakuwa mmepoteza kila kitu. Mimi nawashauri msichoke kutafuta
majawabu kwa matatizo ya hizi mbili! Huko mnakotaka kwenda kuna hatari nyingi”.
Pengine na ushauri huu wa mtu wa Mungu nao ni vyema kuupa nafasi na
kuutafakari.
Kazi Yenu Kubwa
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Mambo ya kuyasemea ni mengi mno lakini kwa sababu ya ufinyu wa muda,
nisingeweza kuyazungumzia yote. Naamini, mtayaona katika kuipitia Rasimu na
kwenye majadiliano yenu. Napenda kusisitiza kwenu kuwa kazi iliyo mbele yenu ni
kubwa sana. Ni kubwa kwa maana mbili. Kwanza, jukumu lenyewe la kutunga Katiba
ya nchi ni zito sana. Taswira ya nchi yetu itakuwaje na itaendeshwa vipi kwa
miaka mingi ijayo iko mikononi mwenu. Ipeni nchi yetu hatima njema. Pili, ni
kubwa kwa maana ya uzito wa mambo ya kujadili na kuyafanyia uamuzi. Kwa ajili
hiyo, ni muhimu sana kuisoma Rasimu na Taarifa ya Tume kwa makini na kuzielewa.
Jipeni muda wa kutafakari kila neno, kila sentensi, na kila dhana ili muweze
kufanya uamuzi ulio sahihi. Mkifanya hayo mtakuwa mmeisaidia nchi yetu na
Watanzania wote kupata Katiba nzuri.
Nimefarijika sana kusikia kuwa mtajigawa kwenye Kamati 12 wakati wa kujadili
Rasimu. Huu ni utaratibu mzuri kwani mkiwa katika vikundi vya watu wachache,
mtakuwa na mijadala ya kina zaidi. Watu wote wanaweza kupata fursa ya kutoa maoni
yao, kwa kila kifungu na kila jambo linaloibuliwa na kuzungumzwa. Kwa kufanya
hivyo, mtatimiza kwa ukamilifu jukumu lenu la kutunga Katiba. Wote mtakuwa
mmeshiriki kujadili kila sura na vipengele vyake vyote. Mkimaliza kazi yenu
mtapokea kwa haki sifa nzuri kama Katiba itakuwa nzuri, au lawama stahiki iwapo
itakuwa kinyume chake.
Pongezi kwa Mwenyekiti wa Muda
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Nitakuwa mwizi wa fadhila kama nitamaliza hotuba yangu bila ya kutambua kazi
nzuri iliyofanywa na Mheshimiwa Pandu Ameir Kificho, Spika wa Baraza la
Wawakilishi, alipokuwa Mwenyekiti wa Muda wa Bunge hili. Kazi yake haikuwa
rahisi hata kidogo, lakini kwa umahiri na ustadi mkubwa ameweza kufanikisha
mambo kwa kiasi ambacho anastahili pongezi zetu sote. Anastahili pongezi kwa
sababu yeye aliendesha Bunge hili bila ya kuwepo kwa kanuni. Tatizo hili
hatakuwa nalo Mwenyekiti wa Kudumu kaka yangu Mheshimiwa Samuel Sitta.
Napenda pia kuwapongeza Waheshimiwa Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba kwa hatua
mliyofikia. Hata hivyo, mmechukua muda mwingi katika hatua ya awali hivyo hamna
budi kuongeza kasi. Naomba niwakumbushe kuwa mijadala yenu hii inafuatiliwa kwa
karibu sana na Watanzania. Wamewekeza sana matarajio yao kwenu. Hamna budi,
haiba na taswira ya uongozi muionyeshe wakati wote wa kuendesha mijadala yenu
kwa lugha na vitendo vyenu. Wakati wa semina na mjadala wa kupitisha Kanuni za
Bunge hili, baadhi ya wananchi wamekwazika sana na mwenendo wa baadhi ya
Wajumbe. Hawakutegemea kuyaona matendo waliyoyaona mkifanya na kusikia maneno
waliyoyasikia kutoka kwenye vinywa vya baadhi yenu.
Ni matumaini yangu na ya Watanzania wote kuwa hali ile haitajirudia tena katika
awamu hii. Tusiwafikishe mahali Watanzania wakakata tamaa na Wajumbe wao au na
hata chombo hiki muhimu sana kwa mustakabali wao na wa nchi yao. Tutoe hoja
badala ya kupiga kelele (argue don’t shout) au kuzomea. Hakuna haja ya kutumia
lugha isiyokuwa ya staha katika kujieleza. Hakuna haja ya kukingiana ngumi,
kutishiana hili na lile au hata kugombana. Ni utovu wa uungwana usiotegemewa
kutoka kwenu. Tusiwaangushe wananchi wa Tanzania wanaotutegemea sana.
Wekeni Maslahi ya Taifa Mbele
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Ombi langu la mwisho kwenu ni kuwasihi kuwa wakati wote muongozwe na kujali
maslahi mapana ya nchi yetu na watu wake badala ya kujali maslahi yenu binafsi
au ya makundi yenu. Naomba kaulimbiu yenu iwe “Tanzania Kwanza”. Najua kila
mmoja wenu amekuja na maoni yake au atakuwa nayo kwa kila jambo
litakalojadiliwa. Wengine wamepewa misimamo na vyama vyao au makundi yao. Si
jambo baya na ni hatua muhimu ya kuleta mafanikio, kama misimamo hiyo na mawazo
hayo ni ya kujenga.
Hata hivyo, mnachotegemewa kufanya ni kuwa tayari kuwianisha na kuunganisha
mawazo yenu mazuri na ya wenzenu, ili kupata msimamo wa pamoja na uamuzi wa
pamoja ulio bora. Kwa sababu hiyo, hamna budi kuwa tayari kusikiliza mawazo ya
wengine, hata kama ni tofauti na yenu mliyokuja nayo. Tafuteni kilicho chema
kwa yale yanayosemwa na watu wengine hata kama ni watu usiokubaliana nao au
huwapendi au hampendani. Kunaweza kuwepo kitu chenye manufaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti na Waheshimiwa Wajumbe;
Nawaomba muwe hodari wa kushawishi badala ya kulazimisha. Mkifanya hivyo
hamtalazimika kutumia muda mwingi wa kula njama za namna ya kuwazidi maarifa
wale mnaotofautiana nao kwa mawazo. Lazima pia mtafute namna ya kushirikiana na
kuwasiliana na makundi mengine. Msitafute kushindana, hili ni jambo ambalo
lazima wote mtoke hapa mkiwa washindi. Yaani lazima Watanzania wote washinde
kwani wao ndiyo wenye Katiba yao. Nawapongeza viongozi wa vyama vya siasa na
asasi mbalimbali kwa kutambua na kuthamini umuhimu wa kuwa na taratibu za
mawasiliano, mashauriano na ushirikiano. Daima muwe watu wa kutafuta
maridhiano. Mmefanya vizuri katika hatua ya awali. Mmejiwekea taratibu nzuri za
kufanya hayo, tafadhalini zitumieni. Jengeni madaraja imara zaidi katika awamu
hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Naomba nimalize kwa kuwaomba Watanzania wote tukiongozwa na viongozi wetu wa
dini tumuombe Mola wetu ajalie rehema zake ili mchakato wa kutunga Katiba uende
salama. Aliongoze Bunge hili na Wajumbe wake waweze kufanya uamuzi ulio sahihi
na wenye manufaa kwa taifa letu kwa kila watakaloliamua.
Baada ya kusema maneno yangu mengi hayo, nirudie kukushukuru Mheshimiwa
Mwenyekiti kwa kunipa fursa hii adhimu ya kulihutubia Bunge Maalum la Katiba.
Nawatakieni kila la heri na mafanikio mema. Katiba Mpya Inawezekana, Timiza
Wajibu Wako.
Mungu Ibariki Tanzania!
Mungu Libariki Bunge Maalumu la Katiba!
Asanteni sana kwa kunisikiliza!